October 7, 2024

Jinsi unavyoweza kuokoa fedha wakati wa manunuzi

Ni kupitia manunuzi ya kila siku ambayo umekuwa ikiyafanya huku yakikulazimu kulipia vitu vidogo vidogo vikiwemo mifuko ya kubebea bidhaa na huduma za usafirishaji.

  • Jitahidi kununua mfuko wako wa kufanyia manunuzi ya bidhaa. 
  • Nunua chupa maalum ya kubebea maji. 
  • Nunua kontena la kubebea chakula ili kuepuka manunuzi ya vibebeo. 

Dar es Salaam. Umewahi kufikiri kuwa zipo gharama ndogo ndogo ambazo unazipata kila siku kwa kupuuzia kuwa ni fedha ndogo lakini makusanyo yake kwa mwezi huwezi kuamini?

Ni kupitia manunuzi ya kila siku ambayo umekuwa ikiyafanya huku yakikulazimu kulipia vitu vidogo vidogo vikiwemo mifuko ya kubebea bidhaa na huduma za usafirishaji. Dondoo hizi zitakusaidia kupunguza gharama za ziada unazopata wakati wa manunuzi: 

Nunua mfuko maalumu wa kubebea bidhaa

Mkazi wa Dar es Salaam Praxeda Mathias amesema kwa wastani, kila siku hununua mfuko mmoja ili kubebea bidhaa anapokuwa sokoni

Mfuko wa kati huuzwa kwa Sh500 ambao ni sawa na Sh3,500 kwa wiki na Sh168,000 kwa mwaka.

Kwa upande wake Balozi wa Malengo ya Dunia Badru Rajabu amesema yeye hufanya manunuzi kila siku kwa ajili ya nyumbani lakini, kwa miezi mitatu sasa, amekuwa akitumia mfuko mmoja tu kufanya manunuzi hayo.

“Nina mfuko mmoja nyumbani. Nikitaka kwenda sokoni ninaubeba. Ninabana matumizi,” Amesema Rajabu ambaye ndani ya miezi mitatu, ameokoa Sh10,000 ambayo huenda angeitumia kila siku kwa manunuzi ya mifuko ya kubebea bidhaa.

Huenda kila uendao sokoni unanunua mfuko wa S500. ukiununua na kuutumia kila uendapo sokoni, utaokoa Sh168,000 kwa mwaka. picha| Google Images.

Nunua chupa ya maji kwa matumizi ya kila siku

Maji ni uhai. Ili mtu aishi ni lazima anywe maji ya kutosha, japokuwa kiwango cha unywaji hutofautiana kati ya mtu na mtu. Ili kujilinda kiafya baadhi ya watu hulazimika kununua maji ya chupa kila siku na kuachana na maji ya bomba. 

Kwa bei ya kawaida, maji yaliyopo kwenye chupa za plastiki huuzwa Sh500 kwa chupa ya lita moja.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam (TUDARco) Joyce Katto ameiambia Nukta kuwa kwa wastani yeye hunywa walau chupa mbili kwa siku.

Hivyo ni sawa kusema Joyce hulazimika kutumia Sh5,000 kwa siku tano za masomo ambazo anakuwa chuoni. Hesabu hiyo ni sawa na Sh40,000 kwa mwezi.

Endapo Joyce atanunua chupa ya kubebea maji, na kisha kuanzisha tabia ya kuchemsha maji, ataokoa fedha alizokuwa akizitumia awali kununua kimiminika hicho.

Chupa za kubebea maji zinapatikana kwenye maduka mengi na hata kwa machinga na nyingi zinauzwa chini ya Sh10,000. 

Mbali na kuokoa fedha, Joyce ataokoa mazingira.


Zinazohusiana


Nunua kontena kwa ajili ya kubebea chakula chako

Unafahamu kuwa baadhi ya migahawa inayosambaza chakula hutoza Sh200 kwa chakula ambacho kinabebwa yaani “take away”? 

Ukinunua kontena la kubebea chakula chako kila unapoenda kununua, itakupunguzia gharama za kulipia fedha ya kununua kibebeo kila wakati. 

Hata hivyo, utakuwa unaokoa mazingira kwani bila shaka unapokuwa umeagiza “take away” hiyo ambayo mara nyingi huwa imetengenezwa kwa malighafi ya aluminium ambayo huchukua hadi miaka 100 kuoza ikitupwa ardhini. 

Ndiyo! Inaweza ikawa ni pesa ndogo lakini ukiiweka, itakusaidia kufanya mambo mengine yakiwemo nauli za daladala na fedha za kununua vitu gengeni.