November 24, 2024

Magufuli awatoa hofu watalii wanaotembelea Tanzania

Amesema ameshuhudia watalii wakiendelea kuingia nchini kwa wingi jambo linalodhihirisha kuwa kwa sasa Tanzania iko salama.

  • Amesema Corona iko mbali na Tanzania, watalii wanaweza kuingia bila wasiwasi.
  • Aitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuitangaza Tanzania kimataifa. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewatoa hofu watalii wanaokuja Tanzania kwa sababu nchi iko salama dhidi ya ugonjwa wa Corona, huku akiitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuitangaza nchi kimataifa.

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Julai 20, 2020) jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi walioteuliwa wiki iliyopita akiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki amesema kwa sasa Corona iko mbali na Tanzania, watalii wanaweza kuja bila wasiwasi. 

“Corona iko mbali kule, ilimalizwa kabisa. Tuliamua kumuomba Mungu, tukamtanguliza Mungu na Mungu akatusikia. Kila mtalii atakayekuwa anakuja atakuja ataangalia wanyama wake na atarudi akiwa salama,”  amesema Dk Magufuli.


Zinazohusiana


Amesema ameshuhudia watalii wakiendelea kuingia nchini kwa wingi jambo linalodhihirisha kuwa kwa sasa Tanzania iko salama.

“Nimeanza kuona watalii wanakuja wengi na ndege zinaleta watalii wengi, watu wameshaanza kuangalia na kuuona ukweli kwamba hapa Tanzania tuko salama,” amesema Dk Magufuli.

Aidha, ameiagiza wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa ili kuvutia watalii wengi zaidi.

Kwa viongozi wengine walioteuliwa, Rais Magufuli amewasisitiza kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi katika maeneo waliyopangiwa kazi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

“Ni bahati nzuri tumeingia kwenye uchumi wa kati. Ni matumiani yangu mtauendeleza huo uchumi wa kati mpaka ukawe uchumi wa juu zaidi. Ni matumaini yangu mtaweza kufanya kazi nzuri,”  ameyasema Rais Magufuli.