November 24, 2024

Unataka biashara ya muungano wa kampuni? Haya yanakuhusu

Hujulikana kama Joint Venture ambayo huunganisha kampuni mbili au zaidi ambazo zinakusanya nguvu zao kuwekeza katika miradi mikubwa.

  • Hujulikana kama Joint Venture ambayo huunganisha kampuni mbili au zaidi ambazo zinakusanya nguvu zao kuwekeza katika miradi mikubwa. 
  • Aina hii ya biashara siyo nzuri kwa wafanyabiashara wachanga na wanaotaka kufanya miradi midogo.
  • Inahitaji chombo maalum cha kuiendesha chenye makubaliano thabiti. 

Leo tunaendelea kuangazia aina za biashara ambazo unaweza kufanya kulingana na mahitaji na malengo yako. 

Muungano wa kampuni (Joint Venture) 

Ni  muunganiko wa kampuni mbili au zaidi  ambazo zinakusanya nguvu zao na  mitaji yao pamoja na kuamua kuwekeza kwenye mradi au biashara fulani. Joint Venture kifupi chake kitatumika kama JV kwenye makala haya ili kurahisisha uelewa. 

JV hutumika kwenye miradi mikubwa ambayo inahitaji uwepo wa nguvu kubwa ili kufanikisha ufanyikaji wa mradi huo. Miradi hii inahitaji nguvu na yenzo za kutosha kuifanikisha, jambo ambalo linaifanya  JV kuwa ni sehemu na njia salama ya kufanikisha mradi husika.

Wajibu na utaratibu wote wa shughuli za JV zinawekwa kwenye nyaraka hadhimu inayofahamika kama “JV Agreement”. Nyaraka hii inaonesha majukumu, utaratibu, ukomo na kazi za kila mdau wa JV.


Misingi ya Joint Venture

JV haianzishwi kwa kukurupuka tu la hasha! Ina misingi yake maalumu ya kuisimamia. Mara nyingi inaanzishwa kwa lengo maalumu ambalo kukamilika kwake kunahitaji nguvu ya makubaliano thabiti. 

Hivyo basi lazima kuwe na misingi thabiti ya kuifanya iweze kufanya kazi kwa ufanisi .

Lengo la JV lazima liwe wazi baina ya wadau ili waweze kuwa pamoja kipindi cha JV inapotekelezwa kwa sababu kukosekana kwa lengo la JV ni sawa na roho bila mwili.

Kipindi au muda wa JV lazima ujulikane. Ni vyema iwekwe wazi kwa washirika wa JV kama ni  muda mfupi au mrefu. Hii inasaidia kuhakikisha wadau wanafanya kazi kwa kuweza kutambua ukomo na safari ya ushirika wao.


Soma zaidi: 


Lazima kuwe na mkataba baina ya washirika wa JV ambao unaongoza shughuli zote.  Kila kitu cha JV kinategemea mkataba unasemaje. Mkataba wa JV ndiyo uhai wa JV yenyewe, ni vyema mkataba ukaandikwa kitaalamu na kukidhi hoja zote ili kuondoa sintofahamu ndani ya JV kwa muda ambao mradi utakua unafanyika.


Sheria zinazosimamia JV

Hakuna sheria pekee ambayo ilitungwa kusimamia JV nchini Tanzania, kwa kiasi kikubwa JV inasimamiwa na Sheria za Mikataba na Kampuni za mwaka 2002 (Law of Contract Act na Companies Act). 

Hoja kuu ni kwamba JV inaendeshwa na sheria ya mikataba ,  ‘JV Agreement” inapaswa kukidhi vigezo vyote vya sheria kama mikataba mingine yote. Sheria ya Kampuni  inaingia kwa sababu muunganiko huu unahusisha kampuni zinazosimamiwa na sheria hii.

JV hutumika kwenye miradi mikubwa ambayo inahitaji uwepo wa nguvu kubwa ili kufanikisha ufanyikaji wa mradi huo. Picha| Mtandao.

 

Ugumu wa JV

Changamoto yake kubwa ni chombo kitakachosimamia shughuli za JV. JV yoyote inaendeshwa na chombo maalumu ambacho kinasimamia shughuli zote za JV kama vile kuajiri, kulipa wafanyakazi, kulipa kodi na kununua mali au kitu chochote kinachohusika na JV. 

Chombo hiki ndiyo injini ya JV na kimepewa jina la “Special Vehicle Purpose”. Kwenye Makala hii tunakiita kwa kifupi kama SPV. SPV hutumika kusimamia shughuli zote za JV.

 SPV ndiyo injini ya JV kuhusu umiliki wa mali, kodi, ardhi, mishahara na mambo mengine yote ambayo yanayohusiana na JV. Uhai na uimara wa SPV ndiyo silaha na msingi wa kuendelea na kusimama vizuri kwa JV.

 Anguko lolote la SPV linaua moja kwa moja maisha ya JV. Wafanyabiashara wengi wameshindwa kutengeneza JV nzuri na kusababisha kufa kwa JV nyingi bila hata kufikia malengo yaliyowekwa.

Ukomo wake uko hivi

Maisha ya JV yanategemea malengo au muda uliotengwa kwa ajili ya shughuli za JV hiyo. Maisha ya JV yanaweza kufika mwisho endapo kama “JV Agreement” ilisema muda maalumu wa maisha ya JV au kama kuisha kwa mradi husika ndiyo mwisho wa maisha ya JV.

 Hivyo basi ukomo wake unaamuliwa na vifungu vilivyowekwa kwenye “JV agreement”.

Baadhi ya muungano wa kampuni ambao umekuwepo kwa muda mrefu duniani ni pamoja na kampuni ya Uber na Volvo; Google na Nasa; Renault na Nissan; Sonny na Ericsson. 

Aina hii ya biashara siyo nzuri kwa wafanyabiashara wachanga na wanaotaka kufanya miradi midogo. Uendeshaji wake hasa wa SPV ni mkubwa na unahitaji watu ambao wameshakomaa na kufanikiwa kibiashara tayari.

Wafanyabishara wadogo wanapaswa kuanza na kampuni au ushirika.

Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule

Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini

Kwa msaada wa kisheria wasiliana nami kupitia Twiter: @Hamzaalbhanj , namba ya simu: 0717521700