Serikali yavibana viwanda vya chai vya Mo Dewji
Ni vya kuchakata chai vya Chivanjee na Musekera vilivyopo wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya ambavyo vimefungwa kwa sababu ya uharibifu wa miundombinu na kushindwa kujiendesha.
- Ni vya kuchakata chai vya Chivanjee na Musekera vilivyopo wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya.
- Viwanda hivyo vimefungwa kwa sababu ya uharibifu wa miundombinu na kushindwa kujiendesha.
- Serikali yavitaka vieleze mkakati wa kujiendeleza kabla ya Julai 30, 2020.
Dar es Salaam. Serikali imeagiza kampuni ya Mohamed Enteprises (MeTL) inayomiliki shamba na viwanda viwili vya chai vilivyopo wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya kueleza sababu za kusitisha ununuzi wa majani ya zao hilo kutoka kwa wakulima.
Shamba hilo la Tukuyu Tea Estate na viwanda hivyo vya Chivanjee na Musekera vilikabidhiwa tangu mwaka 2001 kwa kampuni ya MeTL ya bilionea Mohammed Dewji ili viendelezwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alieleza Julai 15, 2020 wakati alipotembelea kiwanda cha chai cha Chivanjee, kuwa hajaridhishwa na sababu za kufungwa kwa viwanda ambavyo vimesitisha ununuzi wa majani mabichi ya chai na uchakataji toka Aprili mwaka huu hali inayoathiri wakulima wa Rungwe.
“Binafsi sijashawishika kama kampuni ya MeTL ina jitihada za makusudi za kufungua viwanda hivi vya Chivanjee na Musekera ili wakulima wa chai wapate soko na nchi ipate mapato yake,” amesema Kusaya.
Mwakilishi wa kampuni ya MeTL George Mwamakula amesema sababu iliyosababisha kiwanda cha Chivanjee kusitisha ununuzi wa chai ni watu waovu kuiba mashine pamoja na miundombinu ya umeme, mota, vyuma na mfumo wa maji wa kiwanda hicho.
Kuhusu kiwanda cha Musekera, amesema imepanga kianze kazi mwaka 2022 baada ya kukamilika kwa ufungaji mitambo mipya na kukarabati miundombinu.
Kiwanda cha chai Chivanjee kilichopo katika shamba la chai Tukuyu kikiwa kimefungwa bila kufanya kazi. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo ameagiza uongozi wa METL kujieleza kwanini umesitisha uzalishaji na ununuzi wa chai ya wakulima kinyume na makubaliano. Picha| Wizara ya Kilimo.
Kusaya atoa agizo zito
Kufuatia hali hiyo, Kusaya amewataka wamiliki wa viwanda kuwasililisha taarifa ya kina inayoonyesha ukubwa wa eneo, kiasi kilichopandwa chai na mikakati ya kampuni hiyo kuendeleza ardhi waliyopewa na Serikali kabla ya Julai 30 mwaka huu.
Sanjari na agizo hilo, Kusaya ameitaka MeTL kuwasilisha taarifa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kabla ya Julai 30 mwaka huu kuelezea mikakati na mpango kazi wa kufufua viwanda vyote viwili.
Iwapo taarifa hizo zitashindwa kuishawishi Serikali, wizara hizo mbili zitamshauri Rais John Magufuli achukue hatua za kuyatwaa mashamba hayo ili apewe mtu mwingine mwenye uwezo wa kuyaendeleza.
Soma zaidi:
- TADB yakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai Iringa
- Soko la chai mbioni kufunguliwa Dar
- Hii ndiyo biashara inayomtesa zaidi bilionea Mo Dewji
Chai yamvuruga pia Mo Dewji
Januari, 2020, Dewji alisema moja ya biashara zake zinazomtesa zaidi na kuwekeza fedha nyingi ni ya kilimo cha chai, jambo linalomfanya aanze kufikiria kuwekeza katika mazao mengine ikiwemo maparachichi.
“Ninajitahidi kutumia muda mwingi katika biashara ya chai. Nimekuwa nikipoteza pesa kwa miaka, tangu kuanzishwa kwake, niwe mkweli. Sasa naangazia kutumia baadhi ya hii ardhi yenye rutuba kwa mazao mengine yenye faida kama maparachichi, ambayo nimeanza kuifanya hivi karibuni,” aliandika mfanyabiashara huyo katika ukurasa wake wa Twitter Junuari 31, 2020.
I’m struggling big time in the TEA business. I’ve been loosing money for years, since inception to be honest. I’m now looking at using some of this fertile land for other lucrative crops like avocado, which I’ve started venturing into recently etc. #AskMoDewji
https://t.co/IY56GwDEx0— Mohammed Dewji MO (@moodewji) January 31, 2020