October 6, 2024

Serikali ya Tanzania yawahakikishia wakulima soko la mazao

Imewahakikishia wakulima kuwa itaendelea kununua mazao yao kwa ajili ya kuongeza hifadhi ya chakula nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akiwa anakagua mfuko unaotumika kuhifadhia mpunga katika kituo cha manunuzi Uturo wilaya ya Mbarali leo. Picha| Wizara ya Kilimo.


  •  Imewahakikishia wakulima kuwa itaendelea kununua mazao yao kwa ajili ya kuongeza hifadhi ya chakula nchini.
  • Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kununua na kuhifadhi mazao hayo.

Dar es Salaam. Serikali imewahakikishia wakulima kuwa itaendelea kununua mazao yao kwa ajili ya kuongeza hifadhi ya kutosha na uhakika na usalama wa chakula nchini Tanzania

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema hayo wakati alipotembelea kituo cha ununuzi wa zao la mpunga katika kijiji cha Uturo wilayani Mbarali unaofanywa na Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kanda ya Makambako. 

“Serikali kupitia wizara ya Kilimo itaendelea kununua mazao ya wakulima hususan mahindi na mpunga kwa wingi hivyo wakulima msidanganywe kuwa muda umebaki mfupi wa kupeleka mazao yenu NFRA. Leteni hapa mpunga wenu tutaununua wote” amesema Kusaya.

Amesema wizara imejipanga kuona nchi inaendelea kuwa na usalama wa chakula ndiyo maana anapita mikoani kujionea hali ya uzalishaji wa mazao mbalimbali.  


Zinahusiana: 


Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makambako Frank Felix amesema tayari wakala umeshanunua tani 1,700 za mpunga kati ya malengo ya tani 5,000 na mahindi tani 2,933.174 kati 25,000 msimu huu. 

Ununuzi huo wa mazao unaofanywa na NFRA utaongeza ushindani wa bei kwa wanunuzi na hivyo kuwafaidisha zaidi wakulima ambao wamewekeza kwenye kilimo. 

Katika hatua nyingine, Kusaya ametembelea  Chuo cha mafunzo ya Kilimo na Mifugo  ( MAMRE) cha Wanging’ombe mkoani Njombe  na kutoa agizo kuwa wanafunzi wanaoshindwa kulipa ada ya mafunzo wasifukuze badala yake utafutwe utaratibu rafiki.

Kusaya alitoa agizo hilo kufuatia malalamiko ya wanafunzi kusema baadhi yao wameshindwa kuendelea na masomo baada ya kushindwa kulipa ada na michango mingine.

 “Vyuo vyote 29 ( 14 vya serikali na 15 vya binafsi) ni vyangu kwani vinalenga kuzalisha maafisa ugani watakaokwenda kuhudumia wakulima nchini. Nitaendelela kuvisaidia bila kuangalia nani  anakimiliki muhimu vitoe mafunzo bora kwa wanafunzi wa kitanzania” amesema Kusaya.