November 24, 2024

Huu ndiyo mkoa wenye shule chache zenye huduma ya maji shuleni Tanzania

Ni mkoa wa Songwe ambao takriban shule saba kati ya 10 za mkoa huo hazina huduma ya maji.

  • Ni mkoa wa Songwe ambao takriban shule saba kati ya 10 za mkoa huo hazina huduma ya maji. 
  • Mkoa wa Kusini Pemba visiwani Zanzibar ndiyo unaongoza kwa shule nyingi zenye maji
  • Uwepo wa maji shuleni unawasaidia kusoma wanafunzi vizuri na kuongeza ufaulu. 

Dar es Salaam. Licha ya umuhimu wa maji kwa wanafunzi, Mkoa wa Songwe umetajwa kuwa na shule chache zaidi zenye huduma za msingi za maji nchini Tanzania ukiwa chini wa wastani wa kitaifa wa asilimia 55.3.  

Huduma za msingi za maji ina maana kuwa shule ina miundombinu ya maji ya kunywa na usafi kutoka kwenye chanzo cha kuaminika ikiwemo maji ya bomba, kisima, maji ya mvua au chupa.

Ripoti ya utafiti ya uwepo wa maji, huduma ya kujisafisha na usafi shuleni (WASH) ya mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Februari 2020 imeeleza kuwa ni asilimia 29.7 ya shule za Songwe ndiyo zina huduma ya maji. 

Hiyo ni sawa kusema takriban shule saba kati ya 10 za mkoa huo hazina huduma ya maji.

Mkoa huo uko chini kidogo ya mikoa miwili ambayo nayo ina shule chache zenye huduma ya maji shuleni ya Simiyu kwa asilimia 33.9 na Rukwa (asilimia 39).  

Licha ya mikoa hiyo mitatu kuwa na shule chache zenye huduma maji, mikoa mingine 12 ya Tanzania iko chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 55.3, jambo linalodhihirisha kuwa zinahitajika jitihada kuwafikishia wanafunzi huduma hiyo.  

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyofanya utafiti katika shule 2,396 Tanzania  umeutaja mkoa wa Kusini Pemba visiwani Zanzibar kushika nafasi ya kwanza kwa kuwa na shule nyingi zenye huduma za maji kwa asilimia 91.9. 

Hiyo ni sawa na kusema shule 9 kati ya 10 za mkoa huo zina huduma za msingi za maji, jambo linalowafanya wanafunzi kuwa katika nafasi nzuri ya kujisafisha na kupata maji ya kunywa kwa ajili ya afya zao.


Zinazohusiana


Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 49.3 ya shule zilizopo vijijini ndiyo zina huduma ya maji ikilinganishwa na asilimia 68.5 ya shule za mjini. 

Wakati huo ripoti hiyo ya WASH imeeleza kuwa ni shule tano kati ya 10 za Serikali ndiyo zina huduma ya maji ukilinganisha na nane kati ya 10 ya shule za watu binafsi.

Nini kifanyike?

Kwa maeneo ambayo yanakabiliwa na uhaba wa huduma za maji shuleni, ripoti hiyo imependekeza kuwa shule ambazo hazina kabisa huduma hiyo ndiyo zipewe kipaumbele wakati wa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya maji. 

“Hii itasaidia kuhakisha mazingira yenye afya na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi. Pia itaongeza mahudhurio na matokeo mazuri ya shule,” imeeleza ripoti hiyo.

Pia wazazi na jamii wametakiwa kuwaelemisha wanafunzi matumizi sahihi ya maji wakiwa shule ili kulinda afya zao na kuwawezesha kusoma vizuri ili kutimiza ndoto za elimu.