November 24, 2024

Virusi vitano vinavyotafuna kimya kimya afya za Watanzania

Ni mtindo mbovu wa maisha ambao humaanisha afya dhoofu na zilizo wazi kushambuliwa na magonjwa ikiwemo kukosa mazoezi, mapumziko, kutokunywa maji ya kutosha na ulaji mbaya wa vyakula.

  • Ni mtindo mbovu wa maisha ambao humaanisha afya dhoofu na zilizo wazi kushambuliwa na magonjwa.
  • Mtindo huo ni kukosa mazoezi, mapumziko, kutokunywa maji ya kutosha na ulaji mbaya wa vyakula. 
  • Njia pekee ya kuvishinda virusi hivyo ni kuzingatia miongozo ya afya. 

Ilikuwa jumatatu moja mujarabu, niko katika darasa maalumu la mafunzo ya afya likitolewa na mkufunzi ambae awali alikua mwalimu wangu nikiwa chuoni. Ni mtaalamu wa masuala ya moyo na mishipa huyu. 

Ananisogelea karibu, huku akiendelea kuelezea mada yake anayofundisha siku hiyo. Ananiambia, Sultan unafahamu ya kwamba kuna kirusi kipya? 

Akilini mwangu nikajua anaamaanisha virusi vya Corona. Nikamwambia ndiyo, nikataja virusi vya Corona vinavyopelekea homa kali ya mapafu ambavyo ni janga la dunia sasa. 

Akacheka akaniambia “Sultan, usikariri maisha”. Kirusi kipya ni magonjwa ya mtindo wa maisha”. Akaishia hapo. Lakini aliniacha katika tafakuri nzito ambayo leo ndiyo imenipa ari ya kuandika makala haya. 

Mtindo wa maisha ni vile tunavyoishi. Yaani milo, kazi, anasa, muingiliano, burudani nk. Kwa lugha rahisi ni namna tunavyoishi kila siku. Mfumo mzima ambao tumejijengea kuyaongoza maisha yetu. 

Afya zetu zinategemea sana mtindo wa maisha. Namna tutakavyokuwa na mtindo bora wa maisha ndivyo ambavyo afya zitakua imara. Vivyo hivyo mtindo mbovu wa maisha humaanisha afya dhoofu na zilizo wazi kushambuliwa na magonjwa.

Mtindo wa maisha ni vile tunavyoishi. Yaani milo, kazi, anasa, muingiliano, burudani nk. Kwa lugha rahisi ni namna tunavyoishi kila siku. Mfumo mzima ambao tumejijengea kuyaongoza maisha yetu. Picha|Mtandao. 

Magonjwa ya mtindo wa maisha

Kitaalamu, tuna magonjwa ambayo yako katika kundi la mtindo wa maisha. Kimsingi magonjwa haya hayaambukizi, wala siyo matokeo ya virusi, bakteria au fangasi. 

Bali ni matokeo ya namna tunavyoamua kuishi maisha yetu. Na haya ndiyo kirusi kipya siku za karibuni. Kwani ni chanzo cha magonjwa sugu, ulemavu, kushindwa kufanya kazi nk. 

Magonjwa haya ni kama kisukari aina ya pili, shinikizo la juu la damu, maumivu ya mgongo, magonjwa ya moyo, figo na ini. Uzito uliokithiri, kiharusi na mengine mengi. 

Yote haya ukiyachunguza mzizi wake ni namna ambavyo watu wameamua kuishi maisha yao ya kila siku. Chaguzi ambazo tumeamua kuzifanya zinaathiri kwa kiwango kikubwa sana afya zetu na uimara wake. 


Zinazohusiana:


Kirusi cha kwanza ni aina ya vyakula

Ulaji wetu umekuwa siyo wa kiasi na usio na uzingatiwaji wa kanuni za lishe. Vyakula ghafi visivyo na virutubisho, vyakula vya haraka vyenye mafuta, vyakula vya kupaki ni mtindo uliojiwekea mizizi. 

Utumiaji wa vyakula vyenye mafuta huongeza athari za magonjwa ya moyo kutokana na mrundikano wa cholesterol (lehemu). Hii huziba mishipa ambapo huongeza uwezekano wa kiharusi. Huiziba mishipa na kusababisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida.

Kirusi cha pili ni uzito uliozidi 

Asilimia kubwa ya watu wa mjini huwa na uzito uliokithiri. Vitambi ni kama mtindo sasa. Matokeo ya kadhia hizi ni kupungua kwa uwezo wa utendaji wa mwili na mwili kuzidiwa. Chanzo kikubwa ikiwa ni ukosefu wa mpango mzuri wa ulaji na ukosefu wa mazoezi.

Jijengee tabia ya kudhibiti uzito kwa kujua ni namna gani wastani wa uzito na urefu wako (BMI) wapaswa kuwa. Hii itakuepushia maumivu ya viungo, miguu na mgongo. 

Kirusi cha tatu ni unywaji wa pombe uliopitiliza

Pombe hutofautiana kiwango cha kilevi, vivyo hivyo athari zake katika mwili. Nimeshuhudia vijana wadogo chini ya miaka 35 wakifika katika vituo vyetu vya usafishaji figo kutokana na kufeli kwa figo. Chanzo kikubwa kikiwa ni ulevi wa pombe kali. 

Vivyo hivyo athari kubwa katika ini. Dhibiti au acha kabisa utumiaji wa pombe. 

Kirusi cha nne ni kutokula mboga mboga na maji

Mboga mboga na matunda pamoja na unywaji wa maji ya kutosha ni muhimu sana katika miili yetu. 

Lakini vinywaji kama juisi za kupaki na soda zikipewa kipaumbele zaidi huleta shida. Mzigo huu katika figo na maini yetu ni uchoshaji wa viungo hivi muhimu kwa maisha yetu. Binadamu hupaswa kunywa walau lita mbili hadi tatu za maji kila siku. 

Ulaji wa mboga za majani na matunda utakusaidia kukuongezea kinga mwilini. Picha|Getty.

Kirusi cha tano ni ukosefu wa pumziko la mwili

Usingizi wa kutosha na kupumzisha mwili vimekuwa ni hadithi kwa watu wengi. Sababu kubwa ikiwa majukumu mengi. Hali hii husababisha uchovu uliokithiri na kukosa umakini wa mwili huku ikiathiri ufanisi wa tishu na mfumo wa kinga mwili.

Kwa leo jamvi langu nalikunjia hapa. Kukunjwa kwa jamvi si mwisho wa maongezi. Rai yangu kubwa ikiwa ni kuzingatia kuwa nakiasi katika kila kitu. Kufanya marekebisho ya afya zetu kwa kuzingatia mitindo bora ya maisha. 

Natamani nisikuone hospitali kwa sababu unaumwa bali kwa sababu umekuja kufanya uchunguzi wa kawaida tu wa afya yako. 

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.