Bangi yaotesha nyasi vibarua vya vigogo Meru
Magufuli ameagiza kung’olewa kwa viongozi hao baada ya shehena za bangi kukamatwa na vyombo vya usalama vya nje ya wilaya hiyo.
- Magufuli ameagiza kung’olewa kwa viongozi hao baada ya shehena za bangi kukamatwa na vyombo vya usalama vya nje ya wilaya hiyo.
- Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa viongozi waliopo wilayani humo hawatimizi majukumu.
- Agizo ni kuwa wasiishie kuondolewa tu madarakani, ikiwezekana washushwe vyeo.
Dar es salaam. Rais wa Tanzania Dk John Magufuli ameagiza kuondolewa kwa viongozi wawili wa vyombo vya usalama wilaya ya Meru Mkoani Arusha akiwemo Mkuu wa Polisi wilayani humo kwa kutokutimiza wajibu wao ipasavyo.
Dkt Magufuli ametoa maagizo hayo Jumatatu (Julai6, 2020) wakati akiapisha viongozi wateule wakiwemo Kamishna Jenerali Mteule wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya, wakuu wa mikoa na wilaya walioteuliwa hivi karibuni.
“Mnapita kwenye mji unakuta magunia ya bangi, unaenda kwenye mji mwingine unakuta magunia ya bangi na madawa ya kulevya. Hii inaonyesha kwamba kuna kasoro kidogo kwa viongozi wanaoniwakilisha kule,” amesema Dk Magufuli.
Vyombo vya usalama vimekamata bangi kilogramu 188,489 kati ya mwaka 2015 hadi kufikia Juni 2020. Picha| Daniel Samson.
Kufuatia kukamatwa kwa madawa ya kulevya wilayani humo na aliyekuwa Kaimu wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, James Kaji, Rais Magufuli ameagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo (OCD), Mkuu wa Usalama wa wilaya hiyo (DSO) pamoja na polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi wa wilaya hiyo kuondolewa.
“Wote watoke na ikiwezekana wawe ‘demoted’ (washushwe vyeo) inasikitisha mpaka madawa ya kulevya mtu atoke Dar es Salaam akayaone wakati mkuu wa mkoa yupo, mkuu wa wilaya yupo…,” amesema Rais Magufuli akisisitiza kuwa yote hayo yanatokea kwa sababu baadhi ya wateuliwa hawakutimiza majukumu yao.
Zinazohusiana
Madawa ya kulevya ni moja ya mambo yanayoumiza vichwa viongozi na jamii kutokana madhara yake ikiwemo kuharibu nguvu kazi kwa Taifa hasa pale watumiaji wake wanaposhindwa kufanya kazi na kuwa tegemezi.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, vyombo vya usalama vimekamata bangi kilogramu 188,489 kati ya mwaka 2015 hadi kufikia Juni 2020 ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ya madawa ya kulevya kukamatwa ndani ya kipindi hicho.
Bangi inafuatiwa kwa karibu na mirungi ambapo kilogramu 124,080 zilikamatwa katika kipindi hicho, kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa hivi karibuni.
Dawa za kulevya zimesababisha watuhumiwa zaidi ya 73,000 kukamatwa ndani ya kipindi hicho huku zikiacha zaidi ya waathirika 8,000 wakihangaika kupatiwa matibabu ili warudi katika hali zao za kawaida baada ya kuathirika na matumizi ya dawa hizo.