November 24, 2024

Ahueni ya bei ya mafuta yaanza kuota mbawa Tanzania

Bei mpya za rejareja za nishati hiyo kwa Julai zimeongezeka ikilinganishwa na Juni kutokana na mabadiliko katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

  • Bei mpya za rejareja za nishati hiyo kwa Julai zimeongezeka ikilinganishwa na Juni kutokana na mabadiliko katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 
  • Bei za rejareja za dizeli imeongeza kwa Sh170 mbapo wanunuzi watanunua kwa Sh1,716 kwa lita. 
  • Petroli imeongezeka kwa Sh173 sawa na asilimia 11.38. 

Dar es Salaam. Ahueni waliyoipata watumiaji wa petroli na dizeli Jijini Dar es Salaam kwa mwezi mmoja imeanza kuyeyuka baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za rejareja za nishati hiyo kwa mwezi Julai ambazo zimepanda kwa viwango tofauti. 

Mwezi uliopita, wakazi wa Dar es Salaam walikuwa wakinunua lita moja ya petroli kwa Sh1,520 kwa bei ya rejareja huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh1,546 kwa lita. 

Be ya petroli jijini Dar es Salaam ya Juni ni za chini zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita. 

Mara ya mwisho ya bei kama hiyo ilitangazwa na Ewura Desemba 2009 ambapo bei kikomo ya petroli Dar es Salaam ilikuwa ni Sh1,585 kwa lita wakati elekezi ikiwa ni Sh1,475 kwa lita.

Ewura imetangaza bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Julai 2020 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh173 sawa na  asilimia 11.38. 

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalazimika kutoboa mifuko yao, ambapo watalipia Sh1,693 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia Juni. 

Pia bei ya rejareja ya dizeli imeongeza kwa Sh170 mbapo wanunuzi watanunua kwa Sh1,716 kwa lita.  

“Bei za Mafuta ya taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la tarehe 3 Juni 2020 kwani hakuna shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa mwezi Juni 2020 kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” imeeleza taarifa ya Ewura iliyotolewa Jumanne. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura,  Godfrey Chibulunje katika taarifa hiyo amesema mabadiliko hayo ya bei yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 

Ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli  zimeongezeka kwa Sh172.39 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh169.22 sawa na asilimia 11.90.

Bei hizo zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Julai 1, 2020.


Zinazohusiana


Hata hivyo, wakazi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, wao wataendelea kutumia bei zilizokuwepo Juni kwa kuwa hakukuwepo shehena ya mafuta iliyoingilia Bandari ya Tanga. Hii itawahusu pia wanunuzi wa jumla wa nishati hiyo.

Kwa kuwa hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Mtwara katika mwezi Juni 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya dizeli kwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 3 Juni 2020. 

Ewura imesema kutokana na upungufu wa mafuta ya petroli katika maghala ya mafuta mkoani Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es salaam.

“Bei za rejareja za petroli kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es salaam pamoja na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo hadi mikoa husika,” amesema  Chibulunje. 

Pia kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, Ewura imesema wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika.