November 24, 2024

Serikali yataka ada shule binafsi zilipwe kwa makubaliano ya awali

Shule binafsi zaonywa kutoongeza viwango vya ada.

  • Yawataka wazazi kulipa ada kulingana na makubaliano ya awali ya mwaka wa masomo.
  • Shule binafsi zaonywa kutoongeza viwango vya ada. 
  • Shule zote zitafunguliwa Juni 29, 2020. 

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewataka wazazi wenye wanafunzi katika shule binafsi kulipa ada kulingana na makubaliano yalifikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo huku ikizitaka shule kutoongeza kiwango chochote cha ada shule zitakapofunguliwa wiki ijayo. 

Hatua hiyo ya Serikali ni mwenelezo wa jitahada za kutafuta njia za kudhibiti mkanganyiko uliojitokeza hivi karibuni kati ya wazazi na shule hizo ambapo baadhi yao wametaka kupunguziwa ada kwa sababu wanafunzi wamekaa nyumbani kwa muda mrefu bila kusoma.

Hata hivyo, wamiliki wa shule wamekuwa wakisisitiza kuwa ada inapaswa kulipwa kama walivyokubaliana awali kwa kuwa kiwango hicho hutozwa kwa kuzingatia gharama za uendeshaji na siyo kufundisha watoto pekee huku baadhi wakisisitiza kufikia siku za masomo zilizopotea.  

Shule za msingi na sekondari zinatarajiwa kufunguliwa Jumatatu Juni 29, 2020 baada ya wanafunzi kukaa nyumbani zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la Corona.  

“Ada za shule zilipwe kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo. Wizara inaendelea kusisitiza maelekezo ya awali kwamba kusiwepo na nyongeza yoyote katika kiwango cha ada,”  imeeleza taarifa ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyotolewa leo Juni 26, 2020.


Zinazohusiana:


Wizara hiyo imesema wazazi watakiwa kufahamu kuwa kiwango cha ada wanachotozwa huzingatia gharama za uendeshaji wa shule ambazo ziliendelea kuwepo hata wakati shule zilikuwa zimefungwa ikiwemo mishahara ya watumishi, ankara za maji na umeme. 

Kwa upande wa malipo ya chakula na usafiri, wizara imezielekeza bodi za shule kufanya uchambuzi wa gharama inayopaswa kupungua kwa siku ambazo wanafunzi hawakuwa shuleni.  

“Tathmini hii izingatie ratiba mpya ya mihula iliyotolewa na wizara,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Sylvia Lupembe. 

 Wizara hiyo imeelekeza na kusisitiza kuwa wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari wapokelewe bila vikwazo vyovyote Juni 29 kwa ajili ya kuendelea na muhula wa masomo.