November 24, 2024

Serikali yawatoa hofu wakulima kushuka soko la kahawa duniani

Wametakiwa kutokata tamaa kwa sababu soko litaimarika kadiri ugonjwa wa Corona unavyopungua.

  • Wakulima hao wameanza kupata wasiwasi wa kushuka kwa soko la zao hilo kutokana na athari za janga la Corona.
  • Wametakiwa kutokata tamaa kwa sababu soko litaimarika kadiri ugonjwa huo unavyopungua. 
  • Watakiwa kuendelea na shughuli za uzalishaji wa mazao.

Mbeya. Baadhi ya wakulima wa kahawa  mkoani Mbeya, wameanza kupata wasiwasi wa kushuka kwa soko la zao hilo kutokana na athari za janga la Corona huku Serikali ikiwatoa hofu kuwa waendelee na shughuli za kilimo wakati ikishughulikia suala hilo.

Wakizungumza na Nukta (www.nukta.co.tz) kwa nyakati tofauti,  wakulima wa Kahawa katika bonde la Utengule katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi katika mkoa huo wanasema wanapata hofu hiyo kutokana na shughuli nyingi za kimataifa ikiwemo mipaka bado bado imefungwa.

Mmoja wa wakulima hao, Joseph Mwashitete anasema kahawa ni tofauti na mazao ya chakula kwa maelezo kuwa soko lake la ndani ni dogo kuliko la nje na kwamba wao wanazalisha zao hilo kutokana na hamasa wanayoipata kutokana na soko la nje.

Anasema baadhi ya makampuni kutoka nje ya nchi yamekuwa yakiwakopesha hata pembejeo kwa ajili ya zao hilo lakini kwa sasa kuna hatari ya mikopo hiyo kusitishwa na uzalishaji kuporomoka.

“Mazao ya chakula hata tusipouza huwa tunakula wenyewe, lakini kahawa hata gunia moja mimi na familia yangu hatuwezi kutumia tukamaliza kwa mwaka, sasa mataifa tunayoyategemea ndiyo yanayokabiliwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la Corona,” anasema Mwashitete.

Anasema wasiwasi wanaopata ni kusitishwa kwa safari mbalimbali za kimataifa ikiwemo safari za ndege za abiria.


Soma zaidi:


Naye Nathan Mbwaga, ambaye ni mkulima wa kahawa katika Kijiji cha Itimba, anasema msimu wa kahawa kuanza kuchumwa unakaribia lakini mpaka sasa makampuni yaliyoanza kuonyesha nia ya kwenda kununua ni machache.

Ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa kada zote ili kuwahakikishia soko la zao hilo.

Anasema uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukiongezeka kila mwaka kutokana na mahitaji ya soko la dunia na kwamba kwa sasa wana wasiwasi kuwa hata kiwango cha uzalishaji kitashuka kutokana na kuporomoka kwa soko.

Bodi ya Kahawa Tanzania tayari imetoa tangazo la kufunguliwa kwa msimu wa ununuzi wa kahawa ambalo linatoa mambo ya msingi ya kuzingatia ikiwemo ununuzi kufanyika katika minada ya kanda.

Serikali yasema soko la kahawa litaimarika licha ya athari za COVID-19 kwenye sekta ya kilimo. Picha|Mtandao.

Serikali yatoa hofu wakulima

Hofu waliyonayo wakulima wa kahawa pia inakumbuka wakulima wa mazao mengine lakini Serikali imewataka wasikate tamaa waendelee na shughuli za kilimo. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo la soko  na bei ya mazao itaimarika baada ya kuongezeka kwa ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao nchini, ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa masoko na nchi itauza bidhaa zitokanazo na mazao hayo na si malighafi.

“Kushuka kwa bei ya ufuta kusiwakatishe tamaa na kuwafanya muache kulima kwa sababu bei haijashuka kwa zao hilo tu bali na mazao mengine kama chai, tumbaku, kahawa, chai na mazao mengine. 

“Hali hii imetokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambao umeikumba dunia,” amesema Waziri Mkuu jana Juni 24, 2020 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.

Amesema Serikali inatarajia kwamba kadiri ugonjwa wa COVID-19 unavyoendelea kupungua katika mataifa mbalimbali duniani hali ya bei ya mazao nayo itaimarika, hivyo wakulima waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho ni cha mpito.