October 7, 2024

Nyalandu kuanzisha benki ya vijana akichaguliwa rais Tanzania

Amesema itasaidia vijana kupata mikopo na mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kiuchumi.

  • Benki hiyo itawasaidia kujikwamua kiuchumi.
  • Pia ataboresha sheria ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Heslb).
  • Atarudisha Tanzania isiyokuwa na ubaguzi wa dini, vyama na ukabila. 

Mwanza. Mtia nia ya urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Lazaro Nyalandu amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ataanzisha benki ya vijana ili waweze kujikwamua  kiuchumi.

Nyalandu aliyekuwa akizungumza jijini Mwanza Juni 22, 2020 na wanafunzi wa vyuo mbalimbali na vijana walio nje ya mfumo  wa elimu amesema jambo hilo ni kati ya mambo muhimu  matano anayotamani kuyatekeleza katika siku 100 za kwanza za uongozi wake.

“Tumeshuhudia benki za wakulima, wanawake zikianzishwa lakini benki ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa bado haijaanzishwa, wazo hili litakuwa la kwanza kufanyiwa kazi ili vijana wanaojishughulisha na uvuvi, kilimo na hata wafugaji wanufaike,”amesema Nyalandu. 

Amesema mpango wa Serikali itakayoongozwa na Chadema utasaidia kumwandaa kijana aweze kumudu soko la ajira likiwemo la  Afrika Mashariki.


Zinazohusiana:


Aidha, ataboresha sheria ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Heslb) inayomtaka mwanafunzi kuanza kulipa mkopo huo mara tu anapohitimu elimu badala yake atatoa muda wa siku 90 ndipo waanze kurejesha mkopo huo.

Pia atafuta sheria ya ardhi ili kila mtu awe mmiliki halali tofauti na ilivyo sasa ambayo mmiliki halali ni Rais wa Jamhuri badala yake Rais atapewa umiliki katika milima na mbuga za wanyama.

Nyalandu pia  amesema kwa kushirikiana na viongozi wengine, atarudisha ile Tanzania isiyokuwa na ubaguzi wa dini, vyama na ukabila  na kwamba atatoa uhuru wa vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara muda wowote.

Mbali na hayo pia kiongozi huyo alisema atahuisha utashi na uthubutu kwa Watanzania kuwa wanaweza kwa kujengewa mazingira wezeshi ya kuzifuata ndoto zao.

Nyalandu ni miongoni mwa watia nia 11 wa Chadema ambao wanasubiri kupitishwa na chama cha kugombea urais wa Tanzania.