November 24, 2024

Umejiajiri? Haya yanakuhusu kukufanya kuwa bora

Panga ratiba na mipango inayotekelezeka na tumia muda wako vizuri kwa kila kazi unayofanya.

  • Panga ratiba na mipango inayotekelezeka
  • Tumia muda wako vizuri kwa kila kazi unayofanya.
  • Hakikisha una utulivu wa fikra kukamilisha majukumu yako ya kila siku. 

Dar es Salaam. “Kama Mjasiriamali, mimi ni bosi wangu mwenyewe nina panga ratiba zangu na ninajisimamia mwenyewe kwani maendeleo yangu yapo kwenye mikono yangu,” amesema Jessica Mshama ambaye ni mjasiriamali na Mkurugenzi wa kampuni ya J Sisters.

Jessica anasimamia biashara zaidi ya tano kwa pamoja. Anawezaje kuhakikisha kila kiko sawa ikizingatiwa kuwa amejiajiri na uhuru wa kupanga mambo yake atakavyo? 

Kujiajiri kunakupa uhuru wa kutumia muda kulingana na majukumu uliyonayo, lakini usipokuwa makini unaweza kujikuta unapoteza kila kitu ulichokianzisha katika biashara yako. 

Ufanye nini kuhakikisha unatumia muda wako vizuri ili kazi ulizopanga zinakamilika kwa wakati ili kutimiza malengo uliyojiwekea: 

Andaa orodha ya mambo unayohitaji kufanya kila siku

Jessica amesema ni muhimu kufahamu unafanya nini kila siku. Hiyo itakusaidia kufanya mambo yako katika mpango maalumu huku ukihamasika kila unapomaliza jambo moja hadi jingine.

Wekea alama ya ukamilifu kwa kila kitu unachofanya na kukikamilisha.

“Siku nikiamka naandika kuwa saa fulani natakiwa kuwa super market (dukani), saa fulani natakiwa kuwa saluni, saa fulani natakiwa kuwa kiwandani hiyo inanisaidia kuwa katika mpangilio. 

Kwa kila kitu nitakachomaliza ninatiki kwenye orodha yangu kuwa nimekamilisha,” amesema Jessica.

Kama kazi zako zinahitaji umakini mfano katika kufanya mahesabu, manunuzi ya bidhaa na mengineyo, unashauriwa kufanya kazi hizo wakati umetulia na hauna mawazo mengine. Picha| Black News Channel.

Weka malengo halisi na yanayotekelezeka

Wapo watu ambao wanajiwekea malengo ya kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja lakini mwisho wake wanaishia kufanya machache au kunusa nusa kila moja.

Hali hiyo inapelekea kushinda kukamiisha kazi kwa wakati na kuishia kujilaumu mbeleni.


Zinazohusiana:


Fanya kazi ukiwa na utulivu wa akili na fikra

Kama kazi zako zinahitaji umakini mfano katika kufanya mahesabu, manunuzi ya bidhaa na mengineyo, unashauriwa kufanya kazi hizo wakati umetulia na hauna mawazo mengine.

Jessica amesema “usije kujikuta unaingia hasara kwa kushindwa kuwa na umakini. Badala ya kusaini kutoa 10,000 unasaini 100,000. Patamu hapo.”

Panga likizo zako na hakikisha unafuata ratiba yako

Ni vigumu kuanza kufuata kile ratiba yako inasema. Mara nyingi watu huamua kuwa nitavunja hili kwani karatasi haiwezi kunihukumu.

Pia wewe ni kama wafanyakazi wengine. Hakikisha unajipatia likizo kwani unahitaji mapumziko ili kuongeza ufanisi unapokuwa kazini.