October 7, 2024

Magufuli azungumzia msamaha wa madeni wa IMF

Amelishukuru shirika hilo kwa kutambua hatua za Serikali ilizochukua katika mapambano ya Corona na kuipatia Tanzania ahueni ya malipo ya madeni.

  • Ni msamaha wa madai ya madeni ya Serikali ya Tanzania ya dola za Marekani 14.3 milioni katika taasisi hiyo. 
  • Rais Magufuli amesema fedha hizo zitasaidia kupambana na Corona. 

Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeidhinisha msamaha wa madeni ya Serikali ya Tanzania wa  Dola za Marekani 14.3 milioni inayodaiwa na shirika hilo ili zisadie katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona. 

Fedha hizo zilitakiwa kulipwa na Tanzania kwa IMF ikiwa ni sehemu ya malipo ya madeni inayodaiwa. 

Taarifa ya IMF ya Juni 10, 2020 imesema msamaha huo wa sawa na Sh33.1 bilioni ni wa miezi minne hadi Oktoba 13, 2020 ambapo Tanzania haitalipa malipo ya madeni ya mkopo wake yenye thamani ya kiwango hicho inachodaiwa na shirika hilo. 

“Msamaha huo wa madeni utasaidia kuondoa mahitaji ya ulari wa malipo ya Tanzania yaliyochochewa na janga la Corona,” imeeleza taarifa hiyo. 

Pia imepata ahueni ya kutolipa madeni ya dola za Marekani 25.7 milioni (Sh59.7 bilioni) kati ya Oktoba 14, 2020 hadi Aprili 13, 2022 ili kuipunguzia uzito wa malipo ya madeni na fedha hizo zitumike kwa shughuli za maendeleo. 

IMF imesema janga la Corona limeathiri uchumi wa Tanzania hasa katika shughuli za utalii na kasi yake inaweza kuendelea kushuka zaidi, hivyo msamaha huo utasaidia kupunguza athari hizo. 


Soma zaidi: 


Mwakilishi wa Tanzania katika Baraza la Biashara la Afrika Mashariki Raphael Maganga amesema msamaha huo unamaanisha kuwa fedha zilizopangwa kulipa madeni zitaelekezwa katika shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kutoa huduma za kijamii.  

“Hii ni kupunguza uzito wa malipo ya madeni wakati huu wa Corona ambapo uchumi wa dunia umetikisika sana,” amesema Maganga katika ukurasa wake wa Twitter. 

Akizungumzia msamaha huo, Rais John Magufuli ameishukuru IMF  kwa kutambua hatua za Serikali ilizochukua katika mapambano ya Corona na kuipatia Tanzania ahueni ya malipo ya madeni. 

“Msamaha huu umekuja wakati mwafaka. Nimepanga leo nitamuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa IMF kwa niaba ya Watanzania kumpongeza kwamba wametambua juhudi zetu.

“Fedha hizi tutaendelea kuzitumia kupambana na Corona lakini na kuzishughulikia katika maeneo mengine ambayo yatatusaidia Corona isije tena katika nchi yetu,” amesema Dk Magufuli leo jijini Dodoma. 

Amesema kwa sasa Corona imepungua sana lakini Watanzania wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.