Tanzania kuanza kutumia nguzo za umeme za zege
Hatua hiyo itaokoa Sh67 bilioni ambazo zimekuwa zikitumika kubadilisha na kununua nguzo za miti kila mwaka.
Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akiongea na wadau wa nguzo katika ofisi za Wizara ya Nishati leo (Juni 6, 2020) jijini Dar es salaam. Picha| Tanesco.
- Hatua hiyo itaokoa Sh67 bilioni ambazo zimekuwa zikitumika kubadilisha na kununua nguzo za miti kila mwaka.
- Kutaondoa kero ya kukatika kwa umeme kunakosababishwa na nguzo kuanguka au kubadilishwa mara kwa mara.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itaanza kutumia nguzo za umeme za zege katika miradi yake mbalimbali kuanzia Julai mosi mwaka huu, hatua itakayosaidia kuokoa Sh67 bilioni ambazo hutumika kubadilisha na kununua nguzo za miti kila mwaka.
Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amesema kuwa Serikali imeamua kuanza kutumia nguzo za umeme za zege ili kufanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa saa 24 na kuondoa kero ya kukatika kwa umeme kunakosababishwa na nguzo kuanguka au kubadilishwa mara kwa mara.
Uamuzi huo utaisaidia Serikali kuokoa takriban Sh67 bilioni ambazo zimekuwa zikitumika na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kubadilisha na kununua nguzo kila mwaka.
Soma zaidi:
Aidha, Dk Kalemani amepiga marufuku uingizwaji wa nguzo hizo za umeme toka nje na kuruhusu wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza nchini kutengeneza nguzo za zege.
“Tunao umeme wa kutosha kwa sasa, hakuna sababu ya umeme kukatika katika kwa sababu ya kubadilisha nguzo na pia hakuna sababu ya Tanesco kutumia fedha Sh67 bilioni kubadilisha nguzo huku ni kulipa mzigo wa gharama shirika letu,” amesema waziri huyo wakati akiongea na wadau wa nguzo katika ofisi za Wizara ya Nishati leo (Juni 6, 2020) jijini Dar es salaam.
Mwakilishi wa kampuni ya Lukolo inayojihusisha na utengenezaji wa Nguzo za zege Burton Nsemwa amesema hiyo ni fursa kwa wawekezaji wazawa katika kutoa mchango wao kwa Taifa lengo likiwa ni kusukuma gurudumu la maendeleo.
Matumizi ya nguzo za zege huenda ikawa ni habari mbaya kwa wawekezaji wa nguzo za miti ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu nchini.