Shirika la ndege la Qatar kuanza safari Dar Juni 16
Hatua hiyo huenda ikasaidia kuongezeka idadi ya wageni hasa wa utalii wa kimataifa kutembelea vivutio mbalimbali na kuwaunganisha Watanzania na shughuli za kimataifa.
- Shirika hilo la ndege litaanza safari zake ifikapo Juni 16 baada ya serikali ya tanzania kukulegeza masharti dhidi ya ugonjwa wa Corona.
- Wadau wa biashara na utalii wamesema hali hiyo itasaidia kuongeza kasi kwenye sekta hizo.
Dar es Salaam. Watumiaji wa ndege za shirika la ndege la Qatar sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya shirika hilo kutangaza kuanza tena kufanya safari zake katika jiji la Dar es Salaam ndani ya siku 10 zijazo.
Shirika hilo la Qatar Airways limetangaza kuanza safari zake kuingia Tanzania ifikapo Juni16, 2020 baada ya Serikali ya Tanzania kufungua anga na kulegeza masharti dhidi ya janga la Corona (Covid-19) hivi karibuni.
“Qatar inayo furaha kuanza tena safari zake kuelekea Dar es Salaam Tanzania kuanzia Juni 16. Moja kati ya majiji makubwa Afrika, Dar es Salaam ni kitovu cha Biashara na utalii Afrika Mashariki,” imeeleza taarifa ya shirika hilo kwenye tovuti yake.
Hatua hiyo huenda ikasaidia kuongezeka idadi ya wageni hasa wa utalii wa kimataifa kutembelea vivutio mbalimbali na kuwaunganisha Watanzania na shughuli za kimataifa.
Zinazohusiana
- Shirika la ndege la Emirates lawapa ahueni wafanyabiashara Dar
- Shirika la ndege la Emirates lachukua hatua dhidi ya virusi vya Corona
- Zanzibar yazuia ndege kutoka Italia kujikinga na corona
Wadau wa biashara na usafiri wa anga wamesema hiyo ni hatua nzuri hasa kwa ukuaji wa shughuli za usafiri wa anga Tanzania.
Mwakilishi wa Tanzania katika Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Raphael Maganga katika ukurasa wake wa twitter amesema hatua ya Tanzania kufungua anga kumetoa suluhisho kwa mashairika ya ndege kuchangamkia fursa ya kusafirisha abiria kuwaleta nchini.
Mbali na Tanzania, shirika hilo linaendelea na safari zake katika majiji mengine duniani yakiwemo ya London nchini Uingereza, Milan (Italia) na Melbourne nchini Australia.