November 24, 2024

Hapa ndipo uhalifu unapowaunganisha wapendanao

Nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa yupo mwanamke na kwa Bricke mwanamke huyo ni Anna Brewster anayependa fedha zinazomhusu ziwe na sifuri nyingi mwishoni.

  • Ni katika filamu ya “The Last Days of American Crime” inayowakutanisha watu watatu katika uhalifu.
  • Inaelezea mkakati wa vyombo vya dola kutaka kukomesha uhalifu.
  • Wakati vyombo hivyo vinapanga, wahalifu nao wanapanga kufanya tukio la mwisho yaani kubwa kuliko.

Dar es Salaam. Katika nchi hii bwana, uhalifu umetawala. Majambazi na wezi wanafanya yao mchana kweupe bila hata ya wasiwasi. Kuvamia benki na sehemu zenye mali za thamani ni kawaida katika nchi ya “Marekani”. 

Hata hivyo, Serikali ina mpango wa kulikomesha hilo.

Hapo ndipo vyombo vya dola vinaibuka na teknolojia ambayo inatumia mionzi kuzuia mtu yeyote anayefanya uhalifu. Endapo jambazi au mwizi atafikiwa na sauti na mionzi hiyo, basi anasahau hata kama alikuwa anaiba.

Lakini isichojua Serikali ni kuwa, wakati inapanga, wahalifu nao wanajipanga.

Wakati wa mipango ya Serikali, mrembo mmoja na njemba mbili zinataka kufanya tukio kubwa kuliko.

Graham Bricke (Édgar Ramírez) ambaye amempoteza kaka yake aliyeuwawa na polisi anashawishika kuungana na Kevin Cash (Michael Pitt) ambaye anapanga kujaza lori kwa Sh695 bilioni alizopanga kuziiba kutoka benki kuu.

Naam! Anapanga kutumia teknolojia hiyo hiyo ya Serikali kuiibia Serikali.

Hata hivyo, Nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa yupo mwanamke na kwa Bricke mwanamke huyo ni Anna Brewster. Mwanadada ambaye moyo wake unasuuzika kwa kuona gari ziendazo kasi na mwanaume wake anaingiza pesa zenye sifuri nyingi mwishoni.


Zinazohusiana


Usiku wa tukio unawadia, lori la kubebea kitita hicho cha pesa, linaandaliwa na pale ishara inapotolewa, mambo yanaanza kutaradadi.

Hakuna mtu dhaifu anayeweza kustahimili tukio hilo kubwa kuliko kwenye karne na historia ya Marekani isipokuwa hao watatu.

Je, watafanikiwa kusepa na na pesa walizoiba?

Ni katika filamu ya “The Last Days of American Crime” inayoingia kwenye mtandao wa Netflix leo (Juni 5,2020) ikiwa ni maridhawa kwa wikiendi yako.

Kama umelipia kifurishi chako kwenye Netflix, unaweza kuona jinsi mtu anayehitaji ukuu anavyoshirikiana na mtu anayetafuta kisasi kwenye filamu hii yenye kufaa watu wenye miaka 16 na zaidi.

Wiki ijayo kuna nini? Kaa chonjo.