October 6, 2024

CAG awaweka matatani watumishi watatu Nkasi

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nkasi yatakiwa kuwakamata watumishi watatu wa halmashauri hiyo kwa kula Sh27.6 milioni za makusanyo na kujikopesha bila ya kuziwasilisha benki.

  • Wanadaiwa kula Sh27.6 milioni za makusanyo na kujikopesha bila ya kuziwasilisha benki.
  • CAG aipa Halmashauri hiyo hati ya mashaka kwa utata wa mapato. 
  • TAKUKURU yaagizwa kuwakamata na kuwachukulia hatua. 

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nkasi kuwakamata watumishi watatu wa halmashauri hiyo kwa kula Sh27.6 milioni za makusanyo na kujikopesha bila ya kuziwasilisha benki.

Wangabo ameipa TAKUKURU siku saba kuhakikisha watumishi hao wanarudisha fedha hizo na endapo watashindwa kufanya hivyo basi wafikishwe mahakamnami haraka iwezekanavyo.

“Nimeambiwa hizi fedha zinawahusu watumishi wa halmashauri watatu, mmoja anadaiwa Sh4 milioni, na wengine wawili Sh9 milioni (kila mmoja), imesemwa tu wachukuliwe hatua za kisheria, lakini haikutoa muda, hadi lini hawa watu wawe wamechukuliwa hatua hizo za kisheria?, 

“TAKUKURU mko hapa, kamata hawa watumishi watatu, shughulikeni nao haraka iwezekanavyo kuanzia leo,” amesema Wangabo jana katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa hawajawataja watumishi hao kwa majina na vyeo vyao. 

Kikao hicho kilikuwa kinajadili utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/2019. 


Soma zaidi:


Amesema kwa mujibu wa  CAG kwa mwaka wa fedha 2018/2019, mapato yaliyokusanywa bila ya uthibitisho wa kupelekwa benki katika halmashauri hiyo ni Sh47.7 milioni, kati ya hizo Sh20.1 milioni zimerudishwa. 

Hata hivyo, Wangabo amesema taarifa za mfumo wa ukusanyaji wa mapato hadi Mei 31, 2020 unaonesha makusanyo ambayo hayajapelekwa benki yamefikia Sh53.8 milioni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Suleiman Jafo hivi karibuni katika ziara yake mjini Sumbawanga alimtaka Mkuu huyo wa Mkoa kutumia vyombo alivyonavyo kushughulika na wadaiwa wa fedha za makusanyo ambazo hazikuwasilishwa benki.

Katika halmashauri 185 zilizokaguliwa na CAG, halmashauri 176 zilipata hati inayoridhisha na tisa zilipata hati yenye shaka ikiwemo Halmashauri ya Nkasi.

Halmashauri zilizopata hati yenye shaka zimepoteza sifa za kupatiwa fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.