November 24, 2024

Fursa ya mabilioni kilimo cha alizeti kwa vijana Tanzania

Itawasaidia kuboresha maisha kwa kupata kipato cha kuuza katika viwanda vya ndani vya mafuta ya kula ambavyo vina uhitaji mkubwa.

  • Zao hilo linahitajika katika viwanda vya ndani kuzalisha mafuta ya kula.
  • Vijana watakaowekeza watafaidika na fedha zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi. 
  • Matumizi ya teknolojia ya kisasa na upatikanaji wa pembejeo utasaidia kuongeza uzalishaji. 

Dar es Salaam. Watanzania hasa vijana wametakiwa kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika zao la alizeti ili kuongeza malighafi katika viwanda vya ndani na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje nchi. 

Alizeti ni miongoni mwa mazao ya mbegu za mafuta ambayo hutumika kutengeneza mafuta ya kula katika viwanda mbalimbali lakini uzalishaji wake haukidhi mahitaji yaliyopo nchini Tanzania. 

Inakadiriwa kuwa Tanzania inaagiza tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese na hupoteza zaidi ya Sh443 bilioni kila mwaka kwa kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia pengo la uhaba wa mafuta hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji  Angellah Kairuki amesema hiyo ni fursa kwa Watanzania kuzalisha kwa wingi alizeti ili kuvipatia malighafi viwanda na kuokoa fedha ambazo zinaenda nje ya nchi. 

Amewataka wataalam wa kilimo kutoa elimu kwa umma kuhusu kilimo bora cha zao hilo na kuwawezesha kutumia teknolojia ya kisasa na mbegu bora zitakazosaidia kuongeza mavuno.

Kairuki alikuwa akizungumza  alipotembelea na kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti cha Sunshine kilichopo katika eneo la Zuzu jijini Dodoma.


Soma zaidi:


Kiwanda hicho na vingine bado vina uhitaji mkubwa wa alizeti ili viweze kuzalisha mafuta ya kula kwa wingi lakini hilo halitawezekana kama kilimo cha mazao ya mbegu za mafuta ikiwemo alizeti na michikichi hakitapewa msukumo mkubwa hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

“Ni muhimu kuwekeza zaidi katika alizeti kwa sababu soko lake lipo na hii itatatua changamoto ya kuzalisha kwa uchache na kuwafikia wananchi  wengi na kupata soko la nchi za nje”, amesema Meneja Biashara na Maendeleo wa kiwanda cha SunShine Krishna Urs.

Zao hilo hutegemewa zaidi na wakazi wa mikoa ya Dodoma, Singida na Mbeya kujipatia kipato kinachowawezesha kuendesha maisha na kutunza familia lakini hawafaidiki ipasavyo kutokana  uzalishaji mdogo kila mwaka.

Alizeti ndiyo zao la mbegu za mafuta ambalo huzalishwa kwa wingi nchini  licha ya kuwa uzalishaji wake umekuwa ukipanda na kushuka. 

Mathalan, mwaka 2018 uzalishaji wa alizeti ulifikia tani 768,188 sawa na asilimia 47.7 ya mazao yote ya mbegu za mafuta isipokuwa pamba. 

Hata hivyo, uzalishaji wake ulishuka kwa asilimia 75.3 ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo zilizalishwa tani milioni 3.2.

Kitabu namba 5 cha Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Mbegu za Mafuta baada ya kuvuna kilichotolewa na Wizara ya Kilimo kinaeleza kuwa uzalishaji mdogo wa mazao haya unatokana na wakulima wengi kutozingatia kanuni za kilimo bora ikiwemo matumizi ya mbegu bora, mabadiliko ya hali ya hewa na teknolojia duni.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe hivi karibuni aliiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa mazao ya mafuta yako katika fungu la mazao ya kimkakati ambayo Serikali inakusudia kuyapa msukumo mpya kwa kuzalisha mbegu bora na kuwasaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao.