October 7, 2024

Undani wa sheria ya unyanyasaji wa kijinsia Tanzania

Sheria hiyo maalumu kuhusu makosa ya ngono au kijinsia (Sexual Offences Special Provision Act) ya mwaka 1998 inatoa tafsiri halisi ya unyanyasaji wa kijinsia na adhabu zake.

  • Sheria ya “Sexual Offences Special Provision Act” (sheria maalumu kuhusu makosa ya ngono au kijinsia) ya mwaka 1998.
  • Inaeleza kwa undani dhana ya unyanyasaji wa kijinsia na adhabu zake.

Dunia imekua ikishuhudia matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwa muda mrefu sasa tangu karne za zamani kwa namna tofauti. 

Tanzania kama nchi haiko kwenye dunia yake, vitendo vya unyanyasaji kijinsia vimekua vikiripotiwa sehemu mbalimbali nchini. Lakini kwa miaka yote tangu uhuru hakukuwahi kuwepo sheria inayokataza wazi wazi vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Ilikuwa inatumika Sheria ya Kanuni za Adhabu (The Penal Code) lakini ina mapengo makubwa katika suala la vitendo vya unyanyasasaji kijinsia.

Hali hiyo ilisababisha Bunge la Tanzania kutunga sheria maalumu kuhusu makosa ya ngono au kijinsia. Sheria hiyo ilipewa jina la “Sexual Offences Special Provision Act” ya mwaka 1998.

Sheria inasema nini kuhusu unyanyasaji kijinsia?

Unyanyasaji kijinsiai ni kitendo ambacho kinafanywa na mtu mmoja dhidi ya mwingine kikiwa na lengo na kumnyanyasa kijinsia . 

Maana hii imebeba vitu kama maneno, vitendo au kauli ambazo kwa namna moja au nyingine vinamkera mtu kwa sababu vimefanywa kwa msingi wa jinsia yake. 

Kifungu cha 138D (1) cha Sexual Offences Special Provision Act ya mwaka 1998 kimeenda mbali zaidi na kugusia vitu kama ishara, kumsika mtu kwa nguvu na kupelekea mtu kupata usumbufu. 

Kifungu hiki kinatupa elimu kuwa unyanyasaji wa kijinsia lazima kuwe na kitu au kauli imetoka ambayo imesababisha usumbufu kwa mtendewa lakini kilifanyika tu kutokana na jinsia yake.

Sheria hiyo imepiga hatua zaidi na kusema kuwa ufanyaji wa ishara za vidole au mikono ambazo zinalenga kumkera mtu wa jinsia yoyote basi ni unyanysaji wa kingono ambao haukubaliki. 

Sheria haijawaacha wale wanaokohoa au kupiga mbinja akatizapo mwanamke “aliyejaaliwa na Mungu”. Kifungu cha 138D(2) kimeenda mbali zaidi mpaka kuzuia watu kugusa sehemu za siri za wanawake ambao siyo wao  au kufanya hivyo bila hiari yao.

Kutumia nguvu na kipigo kunaweza kukuweka katika matatizo ya kushtakiwa maana ni miongoni mwa ukatili wa kijinsia. Picha| HelpGuide.org

Waathrika wakubwa ni akina nani?

Bila kificho kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za watu wa masuala ya jinsia, wanawake ndiyo wanaripoti zaid vitendo hivi kuliko wanaume. Wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia kuliko wanaume.

Wawawake wamekua wakikumbwa na kadhia hii mahala pa kazi, kwenye usafiri na hata  kwenye sehemu za starehe. Imekua kawaida na desturi mbaya kwa wanaume kuwanyanyasa wanawake hasa sehemu za starehe kama baa na kumbi za muziki wa usiku” Night Club”.

Usikilizaji wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia

Kwanza itambulike vyema shauri la unyanysaji wa kijinsia linatakiwa lifunguliwe ndani ya siku sitini tangu kutokea kwa tukio husika. Sheria inakataza usikilizwaji wa shauri ambalo limefunguliwa baada ya siku sitini kupita

Hizi ni aina ya kesi zenye usiri na unyanyasaji ndani yake. Hivyo basi kulinda heshima ya mtenda na mtendewa, sheria ikaamua usikilizwaji wake uwe wa siri yaani “In Camera”. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 186 (3) kilichofanyiwa marekebisho na Sheria ya Sexual Offences Special Provision Act ya mwaka 1998 kinatamka bayana kuwa makosa ya unyanyasaji wa kijinsia yatasikilizwa kwa usiri na siyo mahakama za wazi kama mengine.

Kimeenda mbali kwa kusema kuwa hata majina ya mashahaidi hayatakua wazi na hata waandishi wa habari hawataruhusiwa kuchapisha hizo habari magazetini juu ya mwenendo wa kesi hiyo.

Ushaidi wa mtoto utapokelewa kwa namna ya pekee, haitakua lazima uwe unasaidiwa na ushaidi mwingine endapo tu mahakama itajiridhisha kuwa ni ushaidi wa kweli na umetolewa na mtoto ambaye ni mtendewa.


Soma zaidi: 


Tukio maarufu la unyanyasaji wa kijinsia

Aprili Mosi mwaka 1991 raia wa kigeni akiwemo Freitag Walter, Huber Waldermar, C Maurice Boutinon and Fritz Koch walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kumnyanyasa kijinsia na kingono. Mariam Benson.

Kosa lao lilikuwa kumvua nguo na kumpiga picha akiwa mtupu na kumlazimisha kufanya mapenzi na mbwa aliyekua akimilikiwa na watuhumiwa hao.

Adhabu yake ni nini?

Kifungu cha 138D(1) cha sheria ya unyanyasaji kijinsia kimeanishia kuwa mtuhumiwa akitiwa hatiani ni faini isiyopungua Sh200,000 au kifungo au vyote kwa pamoja na kulipa fidia kwa mhanga wa kitendo hicho.

Sio kila tukio la unyanysaji wa kijinsia ni Ubakaji , lakini kila tukio la ubakaji linaangukiakwenye unyanyasaji wa kijinsia.

Makala haya yameandaliwa na Hamza Yusufu Lule, Wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini Tanzania. Anapatikana kwa namba 0717 521700 na Twiter: @Hamzaalbhanj