November 24, 2024

Mbinu za kubaini habari za uzushi kuhusu Corona

Unaweza kuithibitisha habari kwa kutafuta chanzo, kuangalia, lugha iliyotumika na zana za kidijitali ili kujua usahihi wake.

  • Mara nyingi zinatoka katika vyanzo visivyo vya uhakika.
  • Huambatana na shinikizo kubwa la kuwataka watu kusambaza kwa haraka.
  • Huwa na makosa mengi ya uandishi na hazijitoshelezi kwa maelezo.

Ni dhahiri kuwa janga la Corona (COVID-19) limezalisha tatizo jingine la habari za uzushi zinazosambaa kwa kasi kupitia intaneti, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa maneno (SMS). 

Habari hizo zinabeba maudhui yasiyo ya kweli, yasiyofaa, yenye makosa na yenye madhara kwa jamii ikiwemo kuhatarisha afya ya umma. 

Lakini habari za uzushi kwa sehemu baadhi huchanganyika na ukweli jambo linalofanya iwe ngumu kujua ukweli na usahihi wa habari husika kwa sababu wakati mwingine husambazwa na marafiki tunaowaamini na wanafamilia. 

Hata kama umeipata habari hiyo kwa mtu unayemwamini ithibitishe kwanza kabla ya kuanza kuisambaza kwa wengine. Tumia dondoo hizi kuithibitisha (Fact check) habari kama ni ya uzushi au ya kweli:

Angalia chanzo cha habari husika

Wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, zipo mamlaka za Serikali na taasisi za afya ambazo zinatambulika kutoa taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo. 

Unaweza kutembelea tovuti na hata kupiga simu kutoka vyanzo vya uhakika ili kuithibitisha habari hiyo kama ni ya kweli. 

Kwa Tanzania, Wizara ya Afya, Msemaji Mkuu wa Serikali ni miongoni mwa vyanzo vya uhakika kuhusu maendeleo ya Corona.

Tumia habari za Corona zinazotolewa na vyanzo vya uhakika ili kujilinda na uzushi wa mtandaoni. Picha|Mtandao. 

Tazama kwa makini tovuti na logo

Wakati mwingine watu wenye nia mbaya hutengeneza tovuti, akaunti za mitandao ya kijamii feki za taasisi zinazohusika na kutoa taarifa za Corona ili kuifanya jamii iamini kwa haraka habari husika. 

Unaweza kulinganisha tovuti na logo halisi na iliyotumiwa visivyo ili kujua ukweli na kuepuka kutumia taarifa ambayo inaweza kukupotosha. Miongoni mwa taasisi ambazo huigwa tovuti zao ni mashirika ya habari. Hakikisha anuani ni yenyewe mfano, www.nukta.co.tz.

Inakuwa na makosa mengi ya kiuandishi

Habari za uzushi huwa na matumizi mabaya ya lugha ikiwemo makosa ya misamiati na uandishi. Wakati mwingine hutumia herufi kubwa na alama za uandishi zisizo sahihi. 

Makosa hayo yakupe mashaka juu ya habari uliyotumiwa kwa sababu mwandishi mzuri au taasisi ni lazima itazingatia taratibu zote za uandishi inapotoa taarifa. 

Ni muhimu kufahamu kuwa siyo habari zote za uzushi zina makosa mengi ya uandishi. Hapa unahitaji jicho lingine la kuibaini. 


Zinazohusiana.


Akaunti feki za mitandao ya kijamii

Hili ni eneo ambalo hutumika zaidi kusambaza habari za uzushi kwa sababu ndiyo majukwaa ambayo watu wengi hukutana mtandaoni kwa shughuli mbalimbali. 

Baadhi ya watu hufungua akaunti feki za Twitter, Instagram au Facebook zinazofanana na akaunti halisi za taasisi au watu na kuweka ujumbe wa kupotosha kuhusu Corona ili watu waamini kwa haraka. 

Ili kujiweka salama dhidi ya madhara utakayopata wewe na jamii yako, chunguza kwa makini jina la akaunti iliyokutumia husika kabla ya kuanza kusambaza au kuitumia taarifa husika. 

Angalia sera za faragha za akaunti halisi kama zinaruhusu aina ya habari hiyo uliyotumiwa au kusambaza kwenye mitandao ya kijamii. 

Shinikizo kubwa la kusambaza

Habari za uzushi hasa zinawekwa kwenye mitandao ya kijamii, huambatana na shinikizo kubwa la kuwataka watu kusambaza kwa watu wengi kadiri wawezavyo. 

Ukipata taarifa hiyo kabla ya kusambaza kwa ndugu na marafiki, jipe muda kwanza wa kuichunguza kwa kutumia vigezo hapo juu ili kujiridhisha usahihi wake na kupunguza madhara kwa watu wengine. 

Usisambaze ujumbe ambao hauna uhakika nao kuhusu Corona. Ithibitishe kwanza. Picha|Mtandao. 

Tumia zana na tovuti za uthibitishaji habari

Habari za uzushi kuhusu Corona ni vita inayopiganwa kila mahali duniani. Zipo taasisi zinazomiliki tovuti na mitandao ya kijamii kama Nukta Fakti,  APFactCheck and Full Fact ambazo kazi yake ni kubaini habari za uzushi na kuweka wazi ukweli. 

Ukifuatilia tovuti hizo zitakusaidia kujua kwa undani habari zilizopotoshwa. Lakini unaweza kutumia vitafutio vya vitu mtandaoni kama Google Image, Google Explorer ili kufahamu kama habari husika imewekwa katika orodha ya habari za uzushi.

Kujifunza zaidi jinsi ya kutumia zana za kidijitali za kubaini habari za uongo endelea kufuatilia nukta (www.nukta.co.tz), Facebook/Twitter: @NuktaFakti na Instagram: @nuktafakti.