November 24, 2024

Ndege ya kwanza ya watalii kutua Tanzania mwishoni mwa Mei

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema ipo tayari kuanza kupokea watalii wakati wowote kuanzia sasa huku ndege ya kwanza ya watalii itawasili mwishoni mwa mwezi Mei.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani Jijini Dar es Salaam, kuhusu kurejeshwa kwa huduma za utalii nchini, kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB Devota Madachi. Picha|MAELEZO.


  • Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema ipo tayari kuanza kupokea watalii wakati wowote kuanzia sasa.
  • Ndege ya kwanza ya watalii itawasili nchi mwishoni mwa mwezi Mei.
  • Imeandaa mwongozo wa kuzingatiwa ili kuwakinga watalii dhidi ya Corona.

Dar es Salaam.Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema ipo tayari kuanza kupokea watalii wakati wowote kuanzia sasa huku ndege ya kwanza ya watalii ikitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi Mei. 

Hatua hiyo ni baada ya Rais John Magufuli kuruhusu kuendelea kwa shughuli za utalii nchini baada ya kupungua kwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona Tanzania. 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi amewaambia wanahabari leo (Mei 20, 2020) kuwa mwishoni mwa Mei ndege ya kwanza inatarajiwa kutua nchini ikiwa na watalii na tayari wadau wote wa utalii wamekamilisha miongozo mbalimbali inayotakiwa kufuatwa ili kuwakinga wageni na corona.

Amesema Serikali imefanya mawasiliano na ofisi za ubalozi wa Tanzania katika nchi za Israel, China na Malaysia ili kuhamasisha  makundi makubwa ya watalii wa nchi hizo waliopanga kuja nchini mwanzoni mwa mwaka huu kufufua mipango yao ya kutembelea vivutio vya utalii.

Mbali na hatua hizo bodi hiyo imepanga kufanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya kupokelea na kulaza watalii ili kujiridhisha iwapo yana huduma mbalimbali za dharura kulingana na mwongozo ulitolewa na Serikali kuhakikisha kuwa utalii unaendelea kuwa salama.


Zinazohusiana: 


Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo  amesema TTB kwa kushirikiana na sekta binafsi imetengeneza filamu mbalimbali za vivutio vya utalii ili kuhakikisha kuwa shughuli za kutangaza utalii hazisimami kutokana na janga la Corona. 

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wa sekta ya utalii, kujitolea kwa hali na mali kutangaza filamu hizi ambazo zimesaidia kutangaza utalii wa Tanzania duniani, na televisheni zetu za ndani zinaweza kuzipata filamu hizi bure bila malipo hapa TTB ili mkaziongeze kwenye ratiba za vipindi vyenu kama sehemu ya kutoa elimu,” amesema Jaji Mihayo.

Kutokana na athari za Corona, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa idadi ya watalii wanaokuja nchini inatarajiwa kushuka kutoka milioni 1.8 waliotarajiwa mwaka huu hadi kufikia watalii 437,000.

Hiyo ni sawa na anguko la zaidi ya mara nne au asilimia 76.5 ya watalii wote waliotarajiwa kuja nchi kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea mbuga za wanyama na fukwe.