November 24, 2024

Majaliwa awaweka kikaangoni watumishi watatu Temesa

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa Wakala huo ambaye aliandika barua ya kuacha kazi Aprili 6, 2020.

  • Ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa Wakala.
  • Wana tuhuma za upotevu wa Sh780 milioni.
  • Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Japhet Maselle aonywa kutokana na usimamizi wake usioridhisha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa Sh780 million zinazotokana na zabuni.

Majaliwa aliyetoa maagizo hayo leo (Mei 19, 2020) alipotembelea karakana ya mitambo ya TEMESA jijini Dodoma, amewasisitiza watumishi wa wakala huo wafanye kazi kwa uadilifu na Serikali haihitaji wala haitowavumilia watumishi wazembe.

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa Wakala huo ambaye aliandika barua ya kuacha kazi Aprili 6, 2020. 

Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza mtumishi huyo arudishwe kazini ili akajibu tuhuma zinazomkabili.

“Kazi hii imefanywa kwa ushirikiano na Afisa wa benki ya CRDB asiyekuwa muaminifu ambaye naye tutamtafuta hadi tumpate. Fedha hizo zilikuwa kwenye mfumo wa hundi wao wakazibadilisha na kuziweka katika mfumo wa fedha taslimu. Umakini usipokuwepo fedha zote zitakuwa zinaliwa tu,”  amesema Majaliwa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemuonya Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Japhet Maselle kutokana na usimamizi wake usioridhisha was taasisi hiyo kwa sababu alikuwa anajua kuhusu upotevu wa fedha hizo na hakuchukua hatua kwa wahusika.

 “…si mzuri kwenye usimamizi unapenda kuacha watu wanaofanya maovu wakiwemo na watumishi hawa watatu. Mtendaji ulikuwa unajua, ulikuwa hauchukui hatua hadi uliposikia nakuja, hii si sahihi sheria zipo na maelekezo ya Serikali yapo. Upotevu wa Sh780 milioni katika taasisi ni doa,” amesema Majaliwa.

Kutokana na matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa TEMESA, amemuagiza Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akafanye ukaguzi katika wakala huo kutokana na upotevu wa Sh780 milioni zilizotakiwa zipelekwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Zinazohusiana

Majaliwa aagiza mradi wa umeme wa Julius Nyerere ukamilike kwa wakati

Majaliwa: Serikali haifanyi biashara utoaji huduma za maji

Majaliwa azungumzia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania


Wanaodaiwa Madeni na TEMESA nao kikaongoni

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na wakala huo ziwe zimelipa madeni yote katika kipindi cha miezi miwili ili kuiwezsha TEMESA kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Tukishapata Sh25 bilioni TEMESA hii tukapeleka walau bilioni moja moja kila mkoa watanunua mitambo, watanunua vipuri na magari yatatengenezwa kwa haraka. Magari yote ya Serikali lazima yatengenezwe TEMESA kwa sababu ya uhakika wa usalama wake,’ amesema.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wakala huo ufanye maboresho makubwa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sehemu ya magari kwa kuwa inalalamikiwa zaidi hususani suala la utengenezaji wa magari yanayopelekwa.