Zanzibar yapokea mashine moja ya kupima Corona
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepokea mashine moja ya kupima ugonjwa wa virusi vya Corona kati ya tatu zilizoagizwa nchini Korea Kusini.
- Mashine hiyo iliyowasili leo ina uwezo wa kupima watu 288 kwa masaa 24.
- Imepatikana kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo.
- Mashine zingine zinatarajiwa kuingia visiwani humo muda wowote kuanzia sasa.
Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepokea mashine moja ya kupima ugonjwa wa virusi vya Corona kati ya tatu zilizoagizwa nchini Korea Kusini.
Mashine mbili zilizobaki, zinatarajiwa kufika wakati wowote na zitafungwa Unguja na Pemba.
Taarifa ya Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar inaeleza kuwa mashine iliyowasili inatoka Korea Kusini kwa ufadhili wa SMZ na mfanyabiashara maarufu wa Tanzania, Rostam Aziz.
“Mashine hiyo inauwezo wa kutoa majibu ndani ya masaa manane kwa vipimo vya watu 96 hivyo kwa saa 24 ina uwezo wa kutoa majibu ya vipimo 288,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Zinazohusiana:
Kuwasili kwa mashine hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk Ali Mohamed Shein Machi 25 mwaka huu alipofanya ziara kuangalia ujenzi wa maabara ya uchunguzi katika kijiji cha Binguni
Aliiagiza Wizara ya Afya kuanza mara moja ujenzi wa maabara itakayochunguza maradhi yanayosababishwa na virusi (Virology Laboratory) na kuhakikisha ujenzi wa maabara hiyo unakamilika haraka iwezekanavyo ili Zanzibar iweze kuwa na mashine zake za kupima virusi vya Corona.
Hata hivyo, taarifa hiyo haijasema mashine hizo zina thamani kiasi gani.
Hadi sasa, Zanzibar imeripoti visa 134 vya wagonjwa wa COVID-19.
MASHINE YA KUPIMA VIRUSI VYA CORONA YAWASILI Z’BAR pic.twitter.com/v5HXucSSRj
— Idara ya Habari Maelezo Zanzibar (@ya_idara) May 15, 2020