Tala yazungumzia kurudi Tanzania
Sehemu ya ujumbe inasomeka kuwa “Tala imerudi tena kwa mara nyingine baada ya kutotoa huduma kwa muda mrefu” ukiambatana na kiunganishi cha tovuti ambayo mtu akiingia anaweza kupata masharti ya kupata mkopo.
- Ni baada ya kusambaa kwa ujumbe wa kurejea kwake nchini Tanzania mwishoni mwa mwezi Aprili.
- Kigogo wa Tala ameiambia Nukta kuwa hakuna maamuzi yaliyofanywa na kampuni hiyo kurudisha huduma nchini Tanzania.
- Tovuti ambayo iliwekwa kwenye uumbe huo haipatikani kwa sasa.
Dar es Salaam. Kampuni ya kutoa mikopo kwa njia ya simu ya Tala imesema siyo kweli kuwa imerejesha shughuli zake Tanzania kwa sababu haijafanya bado uamuzi kama huo tangu ilipositisha huduma zake Septemba 2019.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ujumbe unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa WhatsApp inayoeleza kuwa Tala imerudi Tanzania na kuwataka watu wachangamkie fursa ya kuomba mikopo kwa njia ya simu.
Sehemu ya ujumbe inasomeka kuwa “Tala imerudi tena kwa mara nyingine baada ya kutotoa huduma kwa muda mrefu” ukiambatana na kiunganishi cha tovuti ambayo mtu akiingia anaweza kupata masharti ya kupata mkopo.
Mkuu wa Masoko Afrika Mashariki wa Tala Kevin Kaburu ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa bado hawajaanza kutoa huduma nchini tangu walipositisha mwaka jana.
Amesema ujumbe unaosambaa mtandaoni kuwahimiza watu waombe mkopo Tala siyo wa kweli na wao hawahusiki nao.
“Tala haijafanya maamuzi ya kurudisha biashara nchini Tanzania. Ujumbe uliosambaa ni feki na haujaandaliwa na Tala,” amesema Kaburu kwa njia ya barua pepe.
Zinazohusiana
- Tala haijaondoka Tanzania, imesitisha huduma kujitathmini
- Wataalam wa uchumi watoa suluhisho la biashara kufungwa Tanzania
- NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa
Hata hivyo, tovuti hiyo ya inayodaiwa ni ya Tala kwa sasa haipatikani na Nukta imebaini kuwa mara ya mwisho kutumika ilikuwa Aprili 30, 2020.
Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo nchini Kenya Septemba 18, 2019 ilisema kusitishwa kwa huduma nchini ni kwa ajili ya kutathmini muelekeo wa kampuni hiyo baada ya kukamilika kwa kipindi cha majaribio ya utoaji wa huduma hizo za mikopo Tanzania.
“Tala haijafanya maamuzi ya kusitisha shughuli zake moja kwa moja. Baada ya majaribio ya bidhaa yetu nchini Tanzania, tumesitisha kutoa huduma na tunafanya tathmini ya utendaji wetu kuona mwelekeo wetu kimasoko,” ilieleza taarifa ya Tala.