Unawezaje kuishi na kila mtu kwenye makazi mapya?
Ni changamoto kujifunza kuishi na watu usiowafahamu pale inapobidi lakini yapo mambo ya kuzingatia ili kuwa kwenye nafasi nzuri kufanya hivyo.
- Itakuwa rahisi kwako endapo utajitambulisha kwenye uongozi wa eneo hilo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii.
- Pia, kwa kuepuka kujimwambafai na kutumia uwezo wako kifedha kama fimbo.
- Ni furaha kuelewana na kuishi vizuri na wanaokuzunguka.
Dar es Salaam. Bila shaka huwa inakuwia vigumu pale unapoanza kazi kwenye ofisi mpya, unapoanza kusoma kwenye darasa jipya, na hata unapohamia kwenye nyumba mpya ambayo inakukutanisha na majirani ambao haujawazowea.
Ni kweli wapo watu ambao hali hiyo inaweza isiwe tabu kwao kwani kujenga mazoea na watu wageni siyo shida kwao lakini wapo watu ambao kwao hali hiyo ni kama mtihani ambao hawajajiandaa kuufanya.
Haupo peke yako, wapo baadhi ya watu ambao hupatwa na hofu au kupungua mwili kila wanapokwenda eneo geni ambalo hawafahamiani na mtu yeyote.
Hata hivyo, yapo mambo ambayo yanaweza kukusaidia kujenga mazoea na watu wanaokuzunguka kwa urahisi endapo utahitaji kwani katika dunia hii huwezi jua ni lini utajikwaa na utahitaji mtu wa kukunyanyua.
Jitambulishe kwenye uongozi wa mtaa wako endapo umehamia kwenye makazi mapya
Hauhitaji kupewa jicho la ugeni pale unapohitaji barua ya utambulisho kutoka kwa Serikali za mtaa wako na hasa mjumbe wako. Ndiyo! Bado kuna wajumbe.
Hakikisha hili linakuwa jambo la kwanza baada ya kukamilisha hatua zako zote za kuhamia kwenye nyumba yako. Mjumbe atakuelekeza wapi pa kupata msaada unapouhitaji na pia atakutambulisha kwa majirani zako.
Shiriki kwenye sherehe, na hata misiba. licha ya uwezo wako kifedha, unahitaji watu wenye nia ya dhatimaishani mwako. Picha| Istock.
Jifunze tamaduni za jamii inayokuzunguka
Endapo jamii unayoenda kuishi nayo huwa na vikao jumuishi, basi hiyo ni taa ya kijani kwenye kujenga urafiki na wanajamii wenzako. Hakikisha unahudhuria vikao hivyo na unashiriki kikamilifu kwenye matukio ya kijamii yakiwemo usafi, sherehe na hata misiba inayotokea kwenye mazingira yako.
Licha ya uwezo wa kifedha ulionao, pendelea kuwa mnyenyekevu kwa wakubwa wako na majirani zako kwani hao ndio wa kwanza kufahamu endapo utapata changamoto yeyote ile.
Shiriki kwenye vikundi
Siyo lazima lakini kama wewe ni mama au binti, una kila sababu ya kuonyesha meno yako kwa tabasamu kwani jamii nyingi huwa na vikundi vya kina mama na mabinti vya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, kabla ya kujiunga, unashauriwa kufanya utafiti na kujiridhisha juu ya ufanisi wa vikundi hivyo kwa kufahamu historia yake na utendaji kazi wake. Vyote hivyo unaweza kuvifahamu kwa kuongea na jirani yako kama anashiriki.
Zinazohusiana
- Hivi ndivyo ninavyotabasamu kwa kila kazi ninayofanya
- Fanya haya kuepuka uvivu kazini
- Mazoezi yanayoweza kuongezea ufanisi kazini
Epuka kujimwambafai
Hata kama wewe ni mwenye gari nzuri kuzidi wote, nyumba nzuri kuzidi wote, na mtanashati kuliko wote kwenye jamii yako iwe kazini na hata nyumbani, usipende kutumia hiyo kama fimbo dhidi ya wanaokuzunguka.
Vitu vyote hivyo unaweza kuibiwa na ukakosa hata wa kukusaidia kuvitafuta. Zaidi, penda kujishusha na changamana na wanajamii wenzako kwani utajiri ni watu na sio vitu.
Kuna zaidi katika maisha endapo una mahusiano mazuri na watu wanaokuzunguka. Watu hao ndio watakaokusaidia katika huzuni na hata furaha.
Rafiki yangu ambaye ni mwanamuziki wa nchini Kenya Ambasa Mandela amewahi kuniambia kuwa amani yake ipo kwa kuwa na utajiri wa watu na siyo mali.
Ilinichukuwa muda kumuelewa lakini nilifahamu baada ya kupitia changamoto ambayo fedha haikuwa suluhisho lakini watu wangu wa karibu walinitatulia.
Hadi wakati mwingine, endelea kusoma Nukta.