Makumbusho ya baharini inayongojewa kwa hamu Australia
Ni makumbusho yenye kuonyesha kazi za sanaa zikiwemo sanamu za mbunifu maarufu Jason deCaires Taylor na kivutio kikubwa cha watalii wanaopenda kupiga mbizi.
- Ni makumbusho yenye kuonyesha kazi za sanaa zikiwemo sanamu za mbunifu maarufu Jason deCaires Taylor.
- Inapatikana chini ya bahari kwa umbali wa zaidi ya futi 50.
- Ni kivutio cha utalii hasa kwa wanaopenda kupiga mbizi.
Dar es Salaam. Ni ajabu vile kazi za sanaa zimekuwa zikituzunguka takribani katika kila kitu kilichopo karibu yetu. Kuanzia simu za mkononi, vitanda, milango na hata nguo zinazokupatia umaridadi, vyote ni kazi ya sanaa.
Ili kutokupoteza kazi za sanaa ambazo zimewahi kuushangaza ulimwengu, huenda hapo ndipo wazo la makumbusho lilipoanzia ili kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinapata fursa ya kujua ni wapi mambo kadha wa kadha yameanzia.
Vyote hivyo vinapatikana ardhini lakini wadau wa utalii nchini Australia wameamua kuja na utalii wa aina yake kupitia makumbusho ijulikanayo kama Museum of Underwater Art (MOUA) ya kwenye miamba mikubwa iliyopo chini ya bahari (Great Barrier Reef).
MOUA ni makumbusho inayoonyesha kazi za sanaa zikiwemo sanamu mashuhuli kuwahi kutengenezwa na mbunifu wa sanamu Jason deCaires Taylor ambaye ameibuka na sanamu mbalimbali zinazotamba kwenye makumbusho za baharini ulimwenguni.
Makumbusho ya baharini inayoendelea kujengwa nchini Austraili. Picha|Mtandao
Siyo sanamu tu, ni mambo mengi yanayoonyeshwa kwenye makumbusho hiyo inayopatikana futi 60 chini ya bahari huku anayofikika kwa boti baada ya mwendo wa saa mbili kutoka jiji la Townsville nchini humo.
Makumbusho hiyo ya aina yake inafikika endapo tu ufundi wako wa kupiga mbizi (diving and snorkering) siyo wa kubabaisha ambapo mtalii atapata nafasi ya kuona sanamu 20 mashuhuli zilizotengenezwa kwa kutumia miamba bahari.
Makumbusho hiyo imetengenezwa mahususi kukabiliana na mawimbi ya baharini huku ikiwekwa kwa ueledi kwenye kina chenye maji safi na mchanga mweupe uliopo kwenye eneo tambalale ili kuruhusu utalii kufanyika kwa urahisi.
Kiwango cha hewa ya oksijeni kinahakikishwa kuwa cha kutosha eneo hilo huku kamera zikirekodi jinsi miamba bahari inavyotengenezwa na viumbe wa baharini waliogeuza eneo hilo kama makazi.
Zinazohusiana:
- Yatakayosaidia kunusuru ajira sekta ya utalii Tanzania
- Utalii wa kimataifa kushuka kwa asilimia 30
- Hivi ndivyo unavyoweza kufanya utalii ukiwa angani Tanzania
Uzinduzi wa makumbusho hiyo ulipangwa kufanyika mwezi huu (Mei, 2020) lakini umeahirishwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Mbali na makumbusho hii, zipo makumbuzho zingine za baharini ambazo nazo zina uzuri wake zikiwemo Molinere Underwater Sculpture Park iliyopo kwenye kisiwa cha Grenada ambayo ina sanamu maarufu ya Vicissitudes yenye taswira ya watoto 16 walioshikiliana kutengeneza duara kuonyesha mnyororo wa maisha.
Pia, makumbusho ya baharini ya Museo Subacuático de Arte iliyopo Mexico yenye sanamu 400 na zinginezo nyingi kote ulimwenguni.