November 24, 2024

Rais Magufuli aikalia kooni maabara kuu inayopima Corona Tanzania

Aeleza namna vipimo vilivyopenyezwa kwa siri katika maabara hiyo vilivyobainisha mapapai, mbuzi kuwa na corona

  • Aeleza namna vipimo vya kiuchunguzi vya maabara hiyo vilivyobainisha mapapai, mbuzi kuwa na corona.
  • Awataka Watanzania kuondoa hofu ila waendelee kuzingatia ushauri wa kiafya kujikinga na corona.
  • Serikali yazungumza na Madagascar kuingiza dawa ya corona nchini.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza kuchunguzwa kwa maabara kuu ya afya ya Taifa baada ya kubainika madudu katika upimaji wa virusi vya corona. 

Dk Magufuli amesema kuwa hivi karibuni Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya Prof Mabula Mchembe, timu yake na vyombo vya ulinzi na usalama walipenyeza baadhi ya sampuli zisizo kama oili ya gari, fenesi, mbuzi, kondo, paipai, kwale na nyinginezo katika maabara hiyo na kuzipa majina ya binadamu bila wahusika kujua lakini majibu yalionyesha baadhi ya sampuli hizo zina corona.

“Sasa wewe kama waziri kashirikiane na wizara ya afya. Mkacheki hiyo maabara ya nchi kuna nini ndani? Kama kuna kitu kama criminal (jinai) kiweze kushughulikiwe kisheria,” amesema Rais Magufuli baada ya kumwapisha Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Augustine Mahiga aliyefariki Mei Mosi mwaka huu.

Amesema pia kama vifaa hivyo vina matatizo ya kiufundi pia lazima vichunguzwe.

“Lakini mbuzi awe na corona, fenesi liwe na corona, papai liwe na corona na ndege kama kwale awe na corona ni lazima pawe na maswali mengi ya kujiuliza sisi kama Watanzania lakini Afrika na dunia nzima ijiulize vizuri kuhusu tatizo hili,” amesema Rais Magufuli.


Zinazohusiana:


“Inawezekana wahusika wa laboratory (maabara) ile wamenunuliwa na mabeberu au hawana utalaamu ‘which is not true’ (kitu ambacho siyo kweli) kwa sababu hii maabara imetumika kwa magonjwa mengine…ama hizi samples zina matatizo kwa sababu hata reagents na swabs (pamba maalum za kitabibu) zinatoka nje ya nchi. Kwa hiyo kuna kitu kinaendelea,” ameongeza.

Kiongozi huyo wa juu wa nchi ametoa wito kwa wale wanaotumia vifaa hivyo vya kupimia corona hasa barani Afrika wachukue sampuli za wanyama au kitu chochote hata ukuta na wazipime, watakuja kuthibitisha anachozungumza.

“Mimi ni mwanasayansi najua nachozungumza na kazi hizi zimefanywa na watu ambao “they are really qualified (wenye weledi wa hali ya juu),” amesema Dk Magufuli.

“Kama mpaka mapapai yanatest positive (yanaonyesha yana corona) basi WHO ina kazi kubwa ya kufanya,” ameongeza.


Uwezekano wa kurudisha ligi

Mbali na kuagiza uchunguzi wa maabara hiyo, Dk Magufuli amesema anafikiria siku zijazo kuruhusu ligi iendelee ili wengine watazame kwenye televisheni.

“Nasubiria kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wangu,” amesema Magufuli katika hotuba iliyorushwa mubashara na Shirika la habari la tafa (TBC Taifa).

Amesema Watanzania wanapaswa kutotishana ila waendelee kuchukua tahadhari zilizotolewa na wataalamu wa afya ili kujikinga na ugonjwa huo hatari.


Serikali yazungumza na Madagascar kuhusu dawa ya corona

Dk Magufuli amedokeza pia kuwa Serikali inazungumza na Madagascar juu ya dawa ya corona iliyotangazwa na nchi hiyo siku za hivi karibuni.

“Ninawasiliana na Madagascar na wameshaandika barua wanasema kuna dawa zimepatikana kule. Tutatuma ndege kule na dawa zitaletwa pia ili Watanzania nao waweze kufaidika nayo. Kwa hiyo sisi Serikali tupo tunafanya kazi usiku na mchana,” amesema.