Corona ilivyodhihirisha umuhimu wa teknolojia sekta ya elimu Tanzania
Kwa Tanzania inatumia programu za simu na kompyuta zinazowawezesha wanafunzi wa shule msingi na sekondari kusoma mtandaoni popote walipo wakati shule zimefunga.
- Matumizi ya teknolojia imekuwa ni njia moja salama kwa wanafunzi kupata elimu bila kuhatarisha afya zao kwa kupata maambukizi ya virusi vya Korona (COVID-19)
- Kwa upande wa Serikali kupitia Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kupitia taasisi ya elimu Tanzania (TET) hawako nyuma katika matumizi ya teknolojia.
Dar es Salaam. Watoaji wa huduma ya elimu kwa njia ya mtandao wameeleza kuwa janga la mlipuko wa virusi vya korona (COVID-19) limeonyesha umuhimu wa teknolojia katika sekta ya elimu inayotakiwa kutumiwa na wanafunzi wote ili kupata maarifa na ujuzi kutimiza ndoto zao.
Kwa Tanzania, baadhi ya wabunifu wamebuni programu za simu na kompyuta zinazowawezesha wanafunzi wa shule msingi na sekondari kusoma mtandaoni popote walipo.
Baadhi ya programu hizo za elimu ni pamoja na Shule Direct , MyElimu na Elimu Tanzania ambazo zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi kujipatia notisi, kufanya majadiliano na kufanya mazoezi mbalimbali ya masomo darasani.
Hivyo basi, baada ya Serikali kufunga shule na vyuo vyote nchini kuanzia Machi 17, 2020 ili kuwakinga wanafunzi na COVID-19 kwa sasa masomo kwa njia ya mtandao yamekuwa kimbilio kwa wazazi na wanafunzi hao.
Akiongea na Nukta Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shule Direct, Faraja Nyalandu amesema kwa wastani, idadi ya wanaotembelea kwa siku katika tovuti ya Shule Direct imeongezeka kutoka watu 39,851 hadi 82,957 kwa kipindi cha miezi mitano yaani Desemba 2019 hadi Aprili 2020.
“Unajua kwa sasa matumizi ya teknolojia imekuwa ni njia moja salama kwa wanafunzi kupata elimu bila kuhatarisha afya zao kwa kupata maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19),” amesema Nyalandu.
Hata hivyo, wabunifu hawa wa teknolojia wamebuni programu zinazoweza kutumiwa na wanafunzi wasiokuwa na intaneti katika simu zao ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika elimu.
Mtandao kama My Elimu umekuwa kipaumbele kwa kuhakikisha zaidi wanafunzi wanafanya majadiliano juu ya masomo kupitia mtandao au nje ya mtandao kwa simu za kawaida.
“Tukishirikiana na WhatsApp na Facebook sasa mwanafunzi anaweza kujipatia notisi na kujadiliana na wenzake, hata hivyo anaweza kushiriki nje ya mtandao kwa kuandika SAJILI kwenda 0745622622,” amesema Given Edward, mwanzilishi wa MyElimu.
Programu za elimu mtandaoni zinaweza kuwasaidia wanafunzi kujifunza masomo ya darasani popote walipo. Picha|Mtandao.
Baadhi ya shule za binafsi zimeweka utaratibu kwa wanafunzi kuendelea kusoma wakiwa nyumbani kwa msaada wa wazazi au walezi wa mtoto. Hivyo wengi wamechagua kusoma kwa kutumia njia ya video kupitia Zoom, Edmond, WhatsApp.
“Sisi tuna vipindi kama kawaida kuanzia saa 7:45 asubuhi hadi 2:00 mchana, na mapumziko ni saa nne na saa sita, na yote tunafanya kwa kutumia mtandao,” amesema mmoja wa wanafunzi wa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Aga Khan.
Baruani Mshale,mkazi wa Makongo, Dar es Salaam ambaye ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma shule ya msingi ameiambia Nukta kuwa, shule anayosoma mwanae, inamtaka mzazi ahakikishe mtoto ana kompyuta mpakato, simu janja, tableti au kompyuta yenye mtandao pamoja na sehemu tulivu ambako mtoto atashiriki masomo bila bughdha.
“Tumetakiwa kulipa awamu ya pili ya ada ili mtoto apate kujifunza masomo hayo ya mtandao.” amesema Mshale.
Baadhi ya wanafunzi ambao hawana fursa ya intaneti wao wameamua kujisomea vitabu na notsi katika makundi kuhakikisha hawapitwi na masomo katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa.
“Mimi kwa sasa nimeenda kuishi kwa rafiki yangu, hivyo tunatumia muda mwingi katika kufanya maswali,” amesema Frank Maskati, mwanafunzi wa kidato cha sita, shule ya Sekondari Tambaza ya jijini Dar es Salaam.
Soma zaidi:
- Mfahamu GIven Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
- Apps za elimu zinazoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
- Apps za elimu zitakazowasaidia wanafunzi 2019
Hata hivyo, Serikali ambayo ndiyo mwangalizi mkuu wa elimu nchini Tanzania, imeanzisha programu ya masomo kwa njia ya redio ambapo wanafunzi wanajifunza masomo kwa njia ya sauti.
Programu hiyo inaendeshwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambapo sasa wanafunzi wanaweza kujifunza masomo ya darasani kupitia redio ya TBC Taifa, Azam Tv, Chanel 10 pamoja na ZBC.
Janga la COVID-19 limetufundisha umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia katika sekta ya elimu ili kuwawezesha watoto kupata elimu popote walipo.
Pia kuwatumia wabunifu kutengeneza mifumo na programu zitakazorahisisha utoaji wa elimu bila kumuacha yeyote nyuma.