Wagonjwa wa Corona Zanzibar wavuka 100
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohammed ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya saba wa Corona na kufikisha idadi ya wagonjwa 105 visiwani humo.
- Ni baada ya kutangazwa kwa wagonjwa wapya saba na kufikisha idadi ya wagonjwa 105.
- Idadi ya wagonjwa hao 105 imeongezeka kutoka 98 walioripotiwa Aprili 24, 2020.
- Wagonjwa 36 wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya dalili zao za maradhi hayo kuondoka.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohammed ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya saba wa Corona na kufikisha idadi ya wagonjwa 105 visiwani humo.
Idadi ya wagonjwa hao 105 imeongezeka kutoka 98 walioripotiwa Aprili 24, 2020.
Mohammed katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 28, 2020) amesema wagogonjwa wote wapya ni raia wa Tanzania na wanatokea Unguja na wanaendelea kupata matibabu.
Kwa wagonjwa hao wapya walioripotiwa leo, Tanzania sasa ina wagonjwa 306 huku Jiji la Dar es Salaam likiendelea kuwa kinara wa ugonjwa huo wa COVID-19 baada ya kuripoti visa 143 hadi Aprili 21, 2020 ikifuatiwa na Zanzibar yenye wagonjwa 105.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Aidha, Mohammed amesema wagonjwa 36 waliokuwa katika vituo maalum vya matibabu wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya dalili zao za maradhi kuondoka ikiwemo homa, kikohozi, kifua kubana na kuumwa kichwa.
“Wagonjwa wote wameendelea kushauriwa kubaki katika nyumba zao kwa muda wa siku 14 huku wataalam wa afya wakiendelea kuwafuatilia kwa karibu kabla ya kuruhusiwa kurudi katika shughuli zao za kawaida za maisha,” amesema waziri huyo.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Pia wanakumbushwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hasa katika masoko na vituo vya daladala.