November 24, 2024

Bajeti mambo ya ndani yashuka kwa mara ya pili mfululizo

Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 imeshuka kwa asilimia 2.4 hadi kufikia Sh899.2 bilioni, ikishuka kwa mara ya pili mfululizo tangu ilivyoanza mwaka 2019/20.

  • Imeshuka kwa asilimia 2.4 hadi kufikia Sh899.2 bilioni mwaka 2020/2021 kutoka Sh921.3 bilioni ya mwaka 2019/2020. 
  • Huu ni mwaka wa pili mfululizo bajeti hiyo inapungua.
  • Katika bajeti ya mwaka 2020/2021 wizara imetenga asilimia nne ya bajeti kushughulikia miradi ya maendeleo. 

Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 imeshuka kwa asilimia 2.4 hadi kufikia Sh899.2 bilioni, ikishuka kwa mara ya pili mfululizo tangu ilivyoanza mwaka 2019/20. 

Bajeti hiyo ilisomwa na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene Alhamis (Aprili 23, 2020) bungeni jijini Dodoma na inakusudiwa kupitishwa leo baada ya Wabunge kuijadili kwa kina. 

Hotuba ya bajeti hiyo inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh921.3 bilioni ili kutekeleza majukumu yake lakini zimepungua hadi Sh899.2 bilioni kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021. 

Hiyo ni sawa na upungufu wa Sh22.1 bilioni au asilimia 2.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu inayoishia Juni. 

Huu ni mwaka wa pili mfululizo bajeti hiyo inapungua.

Mathalani mwaka 2018/19 ilikuwa Sh945.5 bilioni kabla ya kushuka hadi Sh921.3 bilioni mwaka 2019/20.

Bajeti ya mwaka 2020/2021 ndiyo bajeti ndogo zaidi ya wizara hiyo kupitishwa na Bunge katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita iwapo wabunge watakubaliana na mapendekezo hayo leo. 

Wakati bajeti ya wizara hiyo ikishuka, fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zimeongezeka hadi Sh35.5 bilioni mwaka ujao wa fedha kutoka Sh31.9 za mwaka huu wa 2019/2020. 

Fedha zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo kwa mwaka ujao ni sawa na asilimia takriban nne tu ya bajeti yote ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Ongezeko hilo la bajeti ya miradi ya maendeleo limekuja baada ya kushuhudia bajeti hiyo ikishuka kila mwaka tangu mwaka 2016/2017, jambo litakalosaidia miradi inayosimamiwa na wizara hiyo kutekelezwa kwa wakati. 

Wizara hiyo inasimamia taasisi nyeti likiwemo Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). 


Zinazohusiana: 


Vipaumbele vya wizara 2020/2021

Waziri Simbachawene amesema fedha zilizotengwa kwa mwaka 2020/21 zitatumika zaidi katika maeneo ya vipaumbele ikiwa ni pamoja na kudumisha usalama wa raia na mali zao na kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa amani na utulivu.

Amesema watatoa mafunzo kwa maafisa, askari na watumishi raia na kuwapandisha vyeo katika ngazi mbalimbali na kununua vitendea kazi tisa muhimu hususan magari. 

“Tutaendelea na ujenzi wa makazi ya askari na ofisi ikiwemo kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Jijini Dodoma,” amesema waziri huyo.

Maeneo mengine ya kipaumbele ni kuendelea na usajili na utambuzi kwa lengo la kufikia idadi ya wananchi 27.7 milioni, kuandaa Sera ya Taifa ya Zimamoto na Uokoaji na Sera ya Taifa ya Uhamiaji na Uraia. 

Mwaka 2020/2021 utakuwa mahususi kufanya marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Jumuiya, Sheria ya Zimamoto na Uokoaji na Sheria ya Uraia na kuendelea kupunguza msongamano magerezani kupitia taratibu na sheria mbalimbali.

“Tutaendelea kutekeleza mkakati wa kujitosheleza kwa chakula wa Jeshi la Magereza na kusimamia utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na mashirika ya uzalishaji mali ya Jeshi la Polisi na Magereza ili yatimize malengo ya uanzishwaji wake,” amesema Simbachawene. 

*Habari hii imeboreshwa kichwa cha habari na chati.