November 28, 2024

Yatakayosaidia kunusuru ajira sekta ya utalii Tanzania

Benki ya Dunia imetoa mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuokoa ajira na mapato katika sekta ya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemoTanzania kwa kuongeza ubunifu na kuwekeza katika utalii wa kidijitali wakati wa mlipuko wa janga la Corona.

  • Benki ya Dunia yapendekeza kubuniwa kwa vyanzo mbadala vya mapato.
  • Utalii wa kidijitali unaweza kuwa sehemu kuiokoa sekta hiyo.
  • Wafanyakazi waandaliwe utaratibu mzuri kulinda ajira zao.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia imetoa mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuokoa ajira na mapato katika sekta ya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemoTanzania kwa kuongeza ubunifu na kuwekeza katika utalii wa kidijitali wakati wa mlipuko wa janga la Corona.

Kutokana na kuenea kwa virusi hivyo vya COVID-19 vivutio vya utalii katika maeneo mbalimbali duniani vimefungwa kuepuka mikusanyiko, jambo lililoathiri ajira za wafanyakazi wa kampuni za utalii, hoteli, mashirika ya ndege, huduma na waongazaji watalii. 

Takwimu za Baraza la Dunia la Usafiri na Utalii (WTTC) za hivi karibuni zinabainisha kuwa ajira za watu milioni 50 katika sekta ya utalii ziko hatarini kupotea ulimwenguni ikiwa ni anguko la kati ya asilimia 12 na 14. 

Hata hivyo, Benki ya Dunia imesema nchi zinazotegemea utalii kama chanzo kikuu cha mapato na ajira, zina nafasi ya kupunguza makali ya COVID-19 na kuendelea kufaidika na sekta hiyo. 

Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Ushindani wa benki hiyo, Caroline Freud katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni kuhusu biashara ya utalii amesema kipindi hiki ni cha kubuni mikakati na kuchukua hatua za pamoja ili kurejesha sekta ya utalii katika nafasi yake. 

Amesema ubunifu wa vyanzo mbadala vya mapato kwa kutengeneza maudhui yanayoonyesha vivutio vya utalii na kuviuza mtandaoni utawawezesha watalii kufanya shughuli za utalii wakiwa katika maeneo yao. 

Baadhi ya hifadhi za Taifa ikiwemo ya Carlsbad Caverns ya nchini Marekani zimeanza kutoa huduma hiyo ya kuongoza watalii ndani ya hifadhi kidijitali.


Zinazohusiana: 


Pia kampuni na mashirika ya utalii yanaweza kuzungumza na wateja wao ambao tayari waliweka oda na kulipia fedha kwa ajili ya kutembelea vivutio katika maeneo wanayosimamia kuahirisha safari badala ya kuondoa kabisa katika ratiba zao. 

Freud amesema njia hii itasaidia kupunguza hasara ili kuepuka kurudisha fedha zao na badala yake watalii wanaweza kwenda katika vivutio husika baada ya janga la Corona. 

“Jamii na vyama vinavyosimamia vivutio vinapaswa kuchukua hatua za dharura kufunga vivutio na kuwasiliana na wateja wao kuhusu kusitishwa kwa huduma ili kuimarisha uhusiano unaoweza kuwanufaisha wakati mwingine,” amesema mtaalam huyo wa biashara wa Benki ya Dunia. 

Serikali zinaweza kuwapunguzia wafanyakazi wa sekta ya utalii mzigo wa kodi katika kipindi hiki ambacho wengi hawako kazini ili kuwapa ahueni ya maisha. Hili pia linaweza kutumika katika kampuni zinazotoa huduma za utalii.

New Zealand imetangaza vifurushi mbalimbali vya msamaha wa kodi na ruzuku kwa wananchi ili kupambana na matokeo hasi ya COVID-19.

Hoteli na fukwe zilizokuwa zinatumiwa na watalii zimebaki bila watu kutokana na janga la Corona. Picha|Mtandao.

Sambamba na hilo, Freud amesema ianzishwe mifuko ya umma ya fedha kuzisaidia biashara kukabiliana na athari za moja kwa moja za COVID-19.

Akitolea mfano nchi ya Singapore, Serikali imechukua hatua ya kubeba gharama za kuwalipa wafanya usafi wa hoteli hasa za utalii. 

Wafanyakazi ambao tayari wamepoteza ajira wanaweza kusaidia kupata mikopo yenye masharti nafuu na ruzuku kwa ajili kuanzisha biashara zitakazowasaidia kujikimu kimaisha hadi pale janga litakapoisha. 

Freud amebainisha kuwa hatua nyingine kutumia baadhi ya rasilimali za utalii kama hoteli na ndege kwa ajili ya kuwahifadhi wagonjwa wa Corona ili kuharakisha matibabu yao. 

Licha ya hatua hizo kunusuru sekta hiyo, Shirika la Utalii Duniani (WTO) limesema idadi ya watalii wa kimataifa itashuka kati ya asilimia 20 na 30 kutokana na kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya corona. 

Taarifa ya shirika hilo lenye makao yake mjini Madrid Uhispania iliyolewa Machi 26, 2020 inaeleza kuwa kupungua kwa idadi ya watalii kutasababisha hasara zaidi ya dola za Marekani bilioni 300 (Sh693.7 trilioni) katika utalii wa kimataifa.