Majaliwa awaonya wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari akieleza kuwa hakuna upungufu wa bidhaa hiyo nchini Tanzania.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika maombi ya pamoja kuhusu kukabiliana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID – 19 kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, Aprili 22, 2020. Kushoto ni Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Yuda Thaddeo Ruwaichi na kulia ni Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Amesema hakuna upungufu wa sukari na hakuna sababu ya kupandisha bei.
- Apiga marufuku kupandisha bei ya vyakula wakati wa mfungo wa Ramadhan.
- Waziri wa Viwanda na Biashara asema kupanda kwa bei ya sukari kumesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari akieleza kuwa hakuna upungufu wa bidhaa hiyo nchini Tanzania.
Katika maeneo mbalimbali nchini, sukari imekuwa haipatikani madukani na katika maeneo inayopatikana imekuwa ikiuzwa kwa bei juu ikilinganishwa na bei elekezi ya Sh1,800 kwa kilo iliyotolewa na Serikali.
Katika baadhi ya maeneo ya jijini Dar es Salaam ambayo Nukta (www.nukta.co.tz) imetembelea, sukari inauzwa kati ya Sh3,500 hadi Sh4,500 kwa kilo huku baadhi ya maduka yakikosa bidhaa hiyo inayotumika kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Aprili 22, 2020) katika maombi ya kitaifa kuombea nchi dhidi ya janga la Corona (COVID-19) amesema sukari ipo ya kutosha na hakuna sababu ya bei kupanda.
“Hakuna sababu ya sukari kupanda, sukari ipo tena ya kutosha,” amesisitiza Majaliwa huku akisema sukari iliagizwa ya kutosha.
Amesema wapo wafanyabiashara wakiwemo wa sukari ambao wanataka kujinufaisha kwa kupandisha bei ya vyakula katika mfungo wa Ramadhani kwa waumini wa dini ya Kiislamu unaotarajia kuanza wiki hii.
“Nitoe wito kwa wafanyabiashara, wiki hii waislam wanaanza mfungo wa Ramadhan, wafanyabiashara kote nchini wahakikishe vyakula katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani vinauzwa kwa bei ya kawaida bila kupandisha bei,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali inafuatilia kwa karibu bei za vyakula ambapo, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya watapita kukagua masoko ili kuhakikisha bei hazipandi na watakaokiuka maelekezo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.
Zinazohusiana:
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho.
- Wakulima wa korosho wameenza kulipwa-Majaliwa
Aprili 17, 2020 Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema ni kweli sukari imepanda na wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile kwa sababu hakuna upungufu wa bidhaa hiyo.
“Ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na kirusi cha Corona “, alisema Bashungwa.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imetoa vibali vya jumla ya Tani 40,000 kwa kampuni nne za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza Tani 10,000.
Waziri Bashungwa alisema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na itasambazwa katika maeneo mbalimbali.
Aidha, alisema Aprili 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya Tani 10,000 huku kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza jumla tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini.
Mahitaji ya sukari inayotumiwa majumbani ni kiasi cha tani 470,000 ambapo kati ya hizo tani 378,000 zinazalishwa nchini.