October 6, 2024

Hapa ndipo Watanzania hupatia zaidi kipato chao

Ripoti ya utafiti wa masuala ya kifedha ya Finscope ya mwaka 2017 inabainisha kuwa watu wanne kati 10 (asilimia 41) wanategemea shughuli za kilimo ikiwemo uvugaji, uvuvi na kulima kama chanzo cha mapato nchini Tanzania.

  • Shughuli ya kilimo ndiyo inategemewa zaidi na Watanzania kupata kipato kwa asilimia 41.
  • Kazi za msimu na biashara navyo vinawabeba watu wengi. 
  • Kipato kinachopatikana katika shughuli hizo huelekezwa kwenye matibabu, elimu na ujenzi. 

Dar es Salaam. Kama bado unajiuliza ni shughuli gani ambayo Watanzania hutegemea zaidi, basi utafiti umebaini kuwa kilimo ndiyo shughuli inayotegemewa zaidi kama chanzo cha kipato kwa ajili ya kugharimia mahitaji mbalimbali ya familia. 

Ripoti ya utafiti wa masuala ya kifedha ya Finscope ya mwaka 2017 inabainisha kuwa watu wanne kati 10 (asilimia 41) wanategemea shughuli za kilimo ikiwemo uvugaji, uvuvi na kulima kama chanzo cha mapato nchini Tanzania.

Hiyo inatokana na kuwa kilimo imekuwa sekta ambayo inategmewa na sekta mbalimbali nchini kuendesha shughuli zake za uzalishaji, hivyo wananchi wengi wanaona ni fursa kuwekeza katika shughuli za kilimo. 

Wakati asilimia 41 wakitegemea kilimo kupata kipato, asilimia 14 au watu 14 kati ya 100 wanategemea  biashara zao binafsi kama njia ya kujipatia kipato.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa kati ya Aprili na Julai 2017, Biashara hizo hujumuisha wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo na zisizo za kilimo na watoa huduma mbalimbali kwenye jamii. 

Licha ya kilimo kutegemewa na wengi, lakini kazi za msimu (casual labor) nazo zimekuwa zikivutia watu wengi hasa vijana ambao hawana ajira za kudumu ambao huingia katika miradi au mikataba ya muda mfupi kujipatia kipato.


Soma zaidi: 


Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa wanaofanya shughuli hizo ni asilimia 20 au sawa na kusema mtu mmoja kati ya watano nchini.  

Wakati wengine wakijishughulisha, ripoti hiyo inaeleza kuwa lipo kundi la watu lipatalo asilimia 18 ambalo kipato cha kukidhi mahitaji yao huwategemea watu wengine wakiwemo ndugu, marafiki na wanafamilia.

“Asilimia 18 ambao ni tegemezi, wengi wao ni wanawake,” inaeleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo ambao hufanywa na Taasisi ya ukuzaji sekta ya fedha Tanzania (FSDT) kwa ushirika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar.

Ni muhimu kufahamu kuwa wapo ambao wanategemea chanzo zaidi ya kimoja, ambao kwa mujibu wa ripoti hiyo ni asilimia 32 huku waliobaki wao wamejielekeza katika chanzo kimoja. Hii ina maana kuwa takriban mtu mmoja kati ya watatu anategemea zaidi ya chanzo kimoja kusukuma maisha yake.

Hata hivyo, kipato hicho kwa mujibu wa utafiti huo hutumiwa zaidi kulipia gharama za afya, elimu (ada), ujenzi wa nyumba na kuweka akiba.