Corona inavyosambaa nchi za Afrika Mashariki
Ugonjwa huo umeingia katika nchi zote za jumuiya hiyo huku Kenya ikiongoza kwa wagonjwa wengi wanaofikia 281.
- Takriban asilimia 44 ya wagonjwa wapo Kenya.
- Jiji la Dar es Salaam ndiyo kitovu cha COVID-19 nchini Tanzania.
- Burundi na Sudan Kusini ndiyo zina wagonjwa wachache katika ukanda huo.
Dar es Salaam. Licha ya Jiji la Dar es Salaam kuongoza kuwa na wagonjwa wengi wa Corona Tanzania, nchi ya Kenya ndiyo inayoshikiria nafasi ya kwanza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Ugonjwa huo aina ya COVID-19 hauna dawa wala chanjo ambapo mgonjwa hutubiwa kutokana na dalili anazoonyesha.
Dalili hizo ni pamoja na homa kali, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya misuli, vidonda vya koo, kubanwa mbavu na kuumwa kichwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyotolewa Aprili 19, 2020, Tanzania imeripoti kuwa na wagonjwa 170 wa Corona baada ya kutangazwa wagonjwa wapya 23 siku hiyo visiwani Zanzibar.
Idadi ya wagonjwa hao inafanya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu cha COVID-19 baada ya kuwa na wagonjwa 100 kati ya 70 waliopo nchini.
Ugonjwa huo pia umesambaa Zanzibar ambapo sasa imethibitisha visa 58 huku kukiwa na wagonjwa wachache katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Lindi, Kagera, na Pwani.
Ifahamike kuwa hadi kufikia jana EAC yenye nchi sita za Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Sudan Kusini na Burundi zilikuwa na wagonjwa 639 wa Corona.
Waziri wa afya wa Kenya Mutahi Kagwe akitoa taarifa ya wagonjwa wapya 11 waliothibitishwa leo Aprili 20 na kufanya nchi hiyo kuongoza katika EAC kwa wagonjwa wengi wanaofikia 281. Picha| Wizara ya Afya Kenya.
Wakati Dar es Salaam na Zanzibar zikiongoza kwa wagonjwa wengi nchini, basi nchi jirani ya Kenya ndiyo iliyolipoti kuwa na wagonjwa wengi wa ugonjwa huo EAC.
Takwimu za wizara ya afya yaKenya za hadi leo Aprili 20, 2020 nchi hiyo ina wagonjwa 281 ambapo miji iliyoathirika zaidi ni Mombasa na Nairobi au sawa na asilimia 43.9 ya wagonjwa waliobanika ndani ya jumuiya ya EAC.
Idadi hiyo ya maambukizi ya COVID-19 nchini humo ni zaidi ya mara moja ya waliopata virusi hivyo Tanzania ambayo imeshika nafasi ya pili kwa wagonjwa wengi.
Uganda yenye hadi kufikia jana kwa mujibu wa Wizara yake ya Afya imeripoti visa 55 tu vya wagonjwa wa Corona ikiwa nyuma ya Tanzania na Rwanda ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa 147.
Nchi mbili zilizobaki za Burundi na Sudan Kusini zimerekodi kiwango cha chini kabisa cha maambukizi ya COVID-19 katika eneo la jumuiya hiyo tangu ugonjwa huo uanze kuitesa dunia mwishoni mwaka 2019.
Burundi imethibitisha kuwa na wagonjwa watano na wanne wamepatikana nchini Sudan Kusini na ndiyo nchi ambazo hazina hata mgonjwa mmoja aliyepona miongoni mwa waliopona katika ukanda huo.
Licha ya Kenya kuwa maambukizi ya kiwango cha juu katika ukanda huo, imethibitisha kuwa wagonjwa 69 wa Corona wamepona huku Rwanda ikiwa na wagonjwa wengi waliopona wanaofikia 76 kwa takwimu za jana.
Waliopona Tanzania mpaka Aprili 19 ni 11 huku 28 wakipona nchini Uganda.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Vifo na hatua zinazochukuliwa
Mpaka jana Aprili 19, nchi za EAC kwa pamoja zimeripoti vifo 20 vilivyosababishwa na COVID-19 huku vifo saba katika kila 10 vikitokea Kenya.
Kenya ina vifo 14 Tanzania (7), Burundi (1) huku Rwanda na Uganda hazijaripoti kifo hata kimoja.
Hata hivyo, nchi zote sita zimeendelea kuungana na jumuiya ya kimataifa kwa kufuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuchukua tahadhari za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.
Tahadhari hizo ambazo zinawagusa watu moja kwa moja ni kunawa mikono mara kwa mara, kutokugusa macho, pua na mdomo, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.