November 28, 2024

Tunanayotakiwa kujifunza kuhusu janga la Corona

Yapo mengi ya kujifunza kutokana na ugonjwa wa Corona ambayo yataathiri maisha yetu hata baada ya ugonjwa huu lakini tukizingatia kanuni za afya tutatoka salama.

  • Uzingatiaji wa kanuni za afya ikiwemo mazoezi na mlo kamili siyo hiari ni lazima. 
  • Kufanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara.

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu mpaji wa vyote kwa nafasi nyingine adhimu ya kunipa afya na uzima tele kuendelea kutumia kalamu yangu ya uandishi wa afya kuelimisha umma wa Kitanzania. 

Zaidi ya yote ninakuombeeni nyote mnaougua ugonjwa huu na kuwatakieni uponyaji dhabiti na haraka. Kongole zangu za dhati kwa Serikali kwa kuweka juhudi madhubuti katika kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu uletwao na virusi vya COVID-19. 

Katika kipindi hiki ambacho mataifa mbalimbali yakiendelea kupambana kutafuta tiba ama chanjo, katika muktadha mpana kuna mengi ya kujifunza kutokana na ugonjwa huu ambayo yataathiri maisha yetu hata baada ya ugonjwa huu. 

Lakini pia yamekua sehemu ya maisha yetu na kupuuza kwake yameleta shida kiafya hata kabla ya COVID-19. Nataka tuangazie mafundisho machache tunayopaswa kuyachukua kama sehemu ya kuzijenga na kuzijali afya zetu. Nenda pamoja nami tukilikunjua jamvi hili! 

Kinga ya mwili haijengwi ndani ya siku moja. Nimeona baadhi ya watu wakishauriana matumizi ya vyakula, mbegu, mizizi pamoja na matunda katika makundi kadhaa ya mtandaoni lengo ikiwa ni kuongeza kinga ya mwili. 

Watu wengi hatufahamu ya kuwa ujenzi wa kinga ya mwili siyo sawa na kibanda cha kuuzia nyanya. Haukamiliki ndani ya siku moja au mbili. 

Ni matokeo ya tabia na siha katika ulaji wa chakula bora chenye afya pamoja na mazoezi na kuzingatia taratibu za kiafya. Nisinukuliwe kuwa nazuia watu kufanya hivyo, la hasha! Bali nachojaribu kuweka sawa ni kuwa katika mtazamo mzima wa kiafya, ujenzi wa kinga ya mwili ni mlolongo na ni matokeo ya kuzingatia kanuni muhimu za afya. 

Ulaji wa vyakula bora vya matunda, mbogamboga na nafaka pamoja na unywaji wa maji unapaswa kuwa utaratibu wetu wa kila siku maana ndicho kiini cha ujenzi wa kinga ya mwili ambayo hupambana na magonjwa. 

Kunawa mikono hutuepusha na vijidudu viletavyo magonjwa mengi katika miili yetu. Unaonekana utaratibu wa kunawa mikono kama ni mpya. Lakini kimsingi ni utaratibu ambao watu wa afya tumekua tukiusisitiza sana na kueleza umuhimu wake kiafya. 

Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ni muhimu kwani huitakasa mikono na kuifanya iwe salama muda wote. 

Tunashika sehemu mbalimbali na kugusana na watu, lakini je tunanawa mikono kwa usahihi? Magonjwa kama kuharisha na homa ya matumbo ni matokeo ya utaratibu mbovu wa kunawa mikono. 

Hatuna budi kupitia hili kujifunza rasmi sasa kuwa kunawa mikono ni siha njema na inapaswa kuzingatiwa hata baada ya Corona. 


Zinazohusiana:


Ufuatiliaji wa taarifa za kiafya. Wataalamu wa afya hutoa taarifa mbalimbali za kiafya na namna ya kujikinga na magonjwa ikiwemo pia namna ya kuzingatia afya na kuijenga ipasavyo. 

Baadhi ya watu hupuuzia mafundisho haya na kutojali, lakini katika kipindi hiki imekua ni tofauti. Waungwana wengi wanafuatilia taarifa kutoka katika kurasa mbalimbali za afya. 

Tukiendelea na utaratibu huu hata baada ya Corona, uhakika wa kuwa na jamii yenye afya thabiti ni mkubwa maana watu watakua wakijali na kutunza afya zao. 

Funzo lingine muhimu sana ni la kuwa salama wakati wote #StaySafe. Tafsiri ya kuwa salama wakati wote ni pana hasa ukiileta katika muktadha maisha ya kila siku. 

Hili hugusia kila aina ya jambo tunalofanya linalotuzunguka katika ujenzi wa afya zetu. Tuko salama kiasi gani na tunawezaje kuendelea kuwa salama? 

Kufanya uchunguzi wa afya walau mara tatu kwa mwaka. Jamii yetu hufikiria huu utaratibu ni wa kimagharibi. Lakini kiuhalisia ni utaratibu muhimu sana katika kuijenga afya. 

Husaidia kutambua magonjwa mapema kabla hayajawa sugu na kuanza matibabu hasa kama magonjwa ni saratani. Pia hutupatia picha halisi ya mwenendo mzima wa afya zetu kwa wakati huo.

Ugonjwa wa Corona umetuachia funzo kubwa la umuhimu wa kuzingatia kanuni za afya. Picha|UN.

Kuwa na Bima ya Afya. Hili nalo ni mojawapo ya njia ya kuwa salama. Je una bima ya afya? Bima ya Afya hukusaidia wewe kumudu gharama za afya utakapougua. 

Hukupa uhakika wa kutibiwa kituo chochote cha afya na kupata huduma bora. Ni njia ya uhakika ya usalama wa afya yako hata pale unapokua hauna pesa mfukoni. 

Tunazingatia kanuni za afya zitolewazo na wataalamu mbalimbali ikiwemo njia anuai za kuchukua ili kujikinga na afya zetu na kuepuka magonjwa yanayoendana na mitindo wa maisha na yale yanayoepukika? 

Ninapokunja jamvi langu, naendelea kuwasihi nyote kuendelea kuchukua tahadhari za muhimu kujikinga na maambukizi ya Corona. Kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kila wakati, ama kutumia vitakasa mikono. 

Pia kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. Toa taarifa unapoona una dalili zozote za corona huku ukijitenga na watu wengine. 

Nina imani kuwa tutalivuka hili pamoja kama Taifa. Mapambano yanaendelea!