October 6, 2024

Hii ndiyo filamu ya kufungia mwezi Aprili

Chris Hemsworth ambaye unaweza kuwa umemzoea kama Thor amevalia kombati zake huku bunduki na mabomu yake yakiwa tayari kukupatia burudani ya aina yake kupitia App ya Netflix.

  • Ni filamu ya Extraction inayomrejesha muigizaji wa Marekani Chris Hemsworth kwenye ulingo wa filamu.
  • Inahusu visa vya nguli wa madawa ya kulevya wa nchi ya Bangladesh na India.
  • Hemsworth anatarajiwa kumkomboa Ovi ambaye ametekwa na magaidi. Ataweza?

Dar es Salaam. Vita kati ya nguli wa dawa za kulevya wa India na Bangladesh inazidi kuchemka baada ya mtoto wa nguli mmoja kutekwa. 

Kuokoa vuguvugu hilo, kwa mara nyingine, Chris Hemsworth ambaye unaweza kuwa umemzoea kama Thor amevalia kombati zake huku bunduki na mabomu yake yakiwa tayari kukupatia burudani ya aina yake kupitia App ya Netflix

Hali ipo hivi, Shujaa huyo ambaye hutumia muda wake kuwaza na kufanya mipango kwenye kina cha maji marefu ana safari ya kumkomboa mtoto wa nguli wa kuuza dawa za kulevya ambaye ametekwa na mpinzani wake.

Tyler Rake (Hemsworth) ambaye jukumu lake ni kumkomboa Ovi (Rudhraksh Jaiswal) anaanza safari yake iliyosheheni ngumi za kutosha huku mateke yakiwa ni chumvi kwenye safari hiyo.

“Kama unataka kupona, fanya kama nitakavyokwambia,” anasema Rake akimwambia Ovi.

Bahari ya safari hiyo inazidi kuchemka pale safari ya wawili hao inapoanza kufuatiliwa na jeshi la polisi huku magaidi nao wakichukua nafasi yao.


Zinazohusiana


Utamu unazidi kukolea baada ya Rake kuamua kumtelekeza Ovi na kurudi alikotoka.

“Utaniacha mitaani?” Ovi anahoji na huenda amesikia maongezi ya mkombozi wake.

Ni nini kitakuwa tamati ya safari yao hata baada ya chumvi kumwagikia kwenye chai?

Fuatiilia kisa hiki chenye jina la Extraction kilichoongozwa na Sam Hargrave ambaye ni kinara nyuma ya filamu ya Atomic Blonde huku sasa akiunganisha waigizaji nguli wa nchini Marekani na wale wa India. 

Kwenye hii filamu, natumaini Wahindi hawataimba kwa nusu saa. Natania!