November 24, 2024

Unavyoweza kuepuka Corona isitafune pesa zako

Kauli za “nunua hiki hakikisha hukosi kile” kuna wakati zinaweza kukuacha ukiwa umeshika kichwa kwa kuchanganyikiwa.

  • Punguza matumizi ya yasiyo ya lazima na jiwekee akiba.
  • Kama unataka kufanya uwekezaji, basi fanya utafiti wa kutosha. 
  • Fuatilia kwa karibu kujua kinachoendelea ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu ugonjwa wa Corona. 

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa wapo watu ambao wapo kwenye njiapanda ya kifedha hasa katika kipindi hiki ambacho ni vigumu kuitabiri kesho ambapo janga la Corona linaendelea kuitesa dunia.

Matumizi ya pesa yamebadilika huku wengine wakiwa na hofu wafanye nini kipindi hiki kujikinga na janga hilo. 

Kauli za “nunua hiki hakikisha hukosi kile” kuna wakati zinaweza kukuacha ukiwa umeshika kichwa kwa kuchanganyikiwa.

Ufanyie nini fedha zako katika kipindi hiki? 

Mtafiti wa masuala ya uchumi Gabriel Mafie amesema kwa kipindi hiki, ni vizuri kujiepusha na kufanya uwekezaji mkubwa kwani huwezi kufahamu hali itakuaje. 

Mafie ameshauri ni vyema kuhakikisha una kiasi cha fedha cha kutosha ili kikusaidie kwenye dharula inapotokea.

Kujiepusha na matumizi yasiyo na ulazima. Mafie amesema kwanini ununue nguo kwa sasa wakati hauzitumii? Matumizi hayo siyo ya lazima hasa kwa ambao wanafanya kazi wakiwa nyumbani. 

Ni muhimu kukaa na familia yako na kujadili mahitaji ambayo ni ya muhimu ambayo hayatakiwi kukosekana nyumbani. 

Kwa kufanya hivyo, utajiwekea akiba na utakuwa tayari kwa dharula yeyote.


Zinazohusiana


Monica Mahinu ambaye ni mama wa watoto watatu mkoani Shinyanga amesema kwasasa amehakikisha ana kiasi cha kutosha kitakachomuwezesha kununua chakula na kuhudumia familia yake pale hali ya dharura itakapotangazwa.

Monica amesema “kwa ongezeko (la wagonjwa) linaloendela, huwezi kutabiri ni kipi kinaweza kutokea kesho ni muhimu kuhakikisha mahitaji muhimu hayakosekani nyumbani.

Chakula, chumvi na dawa za muhimu ili kujiepushia na safari za hapa na pale.” 

Zaidi, Monica ameshauri watu kufuatilia taarifa zinazotolewa kwani zitawasaidia kufanya maamuzi sahihi. 

“Huwezi kujifungia ndani na usifuatile mambo yanayoendelea nje. Kama una redio, fungulia na sikiliza habari zitakusaidia hata kuamua ni nini ukanunue mapema kabla madukani hakijaisha.” amesema Monica.