Tanzania yaingia tena umoja wa wakurugenzi wa kampuni Afrika
Umoja wa Wakurugenzi Watendaji wa kampuni za sekta binafsi Afrika (The Africa List) umetangaza kuongeza wanachama wapya 34 kutoka Tanzania ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike ili kutoa ujuzi wa kuendesha biashara n
- Ni baada ya kampuni ya 34 ikiwemo Sahara Ventures kuchaguliwa kuwa wanachama wapya.
- Umoja huo wa The Africa List unawakutanisha wakurugenzi wa kampuni binafsi Afrika kujadili jinsi ya kukuza kampuni zao.
Dar es Salaam. Ukuaji wa kampuni hasa zile zinatumia teknolojia kutatua changamoto za jamii, unategemea sana uwezo wa viongozi wake kuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha kuwezesha ufanikishaji wa shughuli za utawala na rasilimali watu.
Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, umoja wa Wakurugenzi Watendaji wa kampuni za sekta binafsi Afrika (The Africa List) umetangaza kuongeza wanachama wapya 34 kutoka Tanzania ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike ili kutoa ujuzi wa kuendesha biashara na kutanua wigo wa kuwafikia watu wengi katika maeneo yao.
The Africa List iliyoanzishwa na taasisi ya maendeleo ya masuala ya fedha ya Uingereza iliyopo chini ya kampuni ya CDC Group huwaleta pamoja watendaji wakuu wa kampuni zinazokuwa kasi barani Afrika kubadilishana uzoefu katika utendaji wa shughuli za kuhudumia jamii.
Taarifa ya The Africa List iliyotolewa leo (Aprili 16, 2020) jijini London, Uingereza imeeleza kuwa wanachama hao wanatoka katika sekta mbalimbali ikiwemo benki, kampuni za simu, vyombo vya habari, afya na usafiri wa anga.
Kampuni zingine za Tanzania ambazo viongozi wake watawakilisha katika jukwaa hilo ni pamoja na benki ya CRDB, Access, Stanbic, Metl Group, Raha Tanzania na Vodacom Tanzania.
Kampuni hizo zitaungana na wanachama wengine 750 waliopo katika nchi za Congo DRC, Ethiopia, Ghana, Tanzania, Uganda na Zambia.
Miongoni mwa faida itakazopata Sahara Ventures iliyoongozwa na Mtanzania Jumanne Mtambalike katika umoja huo ni kupata mtandao wa wataalam na ujuzi wa kuifanya iwe endelevu na kuzisaidia kampuni zingine kukua.
Pia wanachama wapya watapata fursa ya kushiriki mafunzo maalum na warsha zinazolenga kuwajengea uwezo viongozi wa kampuni hizo kuwa wabunifu na maono ya muda mrefu.
Mkuu wa The Africa List, Nieros Oyegun katika taarifa yake amesema katika kipindi hiki, sekta binafsi inahitaji viongozi jasiri na wenye uwezo wa kuendesha kampuni zinazoweza kuchangia ukuaji wa uchumi wa dunia.
“Tunatazamia tutafanya nao kazi kwa ukaribu hasa katika shughuli za maendeleo yao,” amesema Oyegun wakati akiwakaribisha wanachama wapya.
Soma zaidi:
- Safari ya mwisho ya Google Plus
- Miaka 15 ya Gmail ilivyongeza thamani bidhaa za Google
- Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google
Wanachama wapya wanachaguliwa kulingana na mafanikio yao, mipango yao kukua katika taaluma na utayari wao wa kubadilishana uzoefu na wanachama wengine.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, wanachama wanatakiwa kuwa na umri kati ya miaka 30 na 50 huku wakiwa na rekodi nzuri ya kuongoza kampuni katika nchi zao.
Sahara Ventures yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam imekuwa mstari wa mbele kuendeleza ubunifu wa teknolojia na kuzisaidia kampuni zinazochipukia (startups) kukua na kuifikia jamii kwa upana kwa kutumia teknolojia rahisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mtambalike ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa hiyo ni fursa kubwa ya kuingia katika jukwaa linaloaminika Afrika ambalo litatoa fursa ya kufanya kazi na kampuni zenye hadhi ya kimataifa.
Amesema pia itawasaidia kuongeza thamani ya kampuni anayoiongoza kwa sababu itakuwa rahisi kuonana na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika maeneo wanayofanyia kazi nchini.
“Itatuongezea mtandao hasa kwa wabunifu na wajasiriamali ambao tunawasimamia kupata soko la bidhaa zao ndani na kimataifa,” amesema Mtambalike.