October 8, 2024

Ugonjwa wa Corona wazidi kuiandama Dar es Salaam

Dar es Salaam imeendelea kuwa kitovu cha ugonjwa huo baada ya kuwa na asilimia 70 ya wagonjwa wote

  • Dar es Salaam imeendelea kuwa kitovu cha ugonjwa huo baada ya kuwa na asilimia 70 ya wagonjwa wote
  • Wagonjwa waliopona hadi sasa wafikia 11 huku waliopoteza maisha wakiwa wanne

Dar es Salaam. Wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Tanzania wamezidi kuongezeka na kufikia 88 baada ya Serikali kutangaza wagonjwa wapya 29, kiwango cha juu kuwahi kuripotiwa kwa siku moja tangu ugonjwa huo uingie nchini katikati ya Machi 2020.  

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema leo kuwa kati ya wagonjwa hao wapya, 26 wapo Dar es Salaam, wawili wapo Mwanza na mmoja yupo mkoani Kilimanjaro.

Idadi ya wagonjwa hao wapya inafanya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu cha COVID-19 baada ya kuwa na wagonjwa 62 kati ya 88 waliopo nchini. Hii ina maana kuwa wagonjwa saba kati ya kila 10 walioripotiwa Tanzania wapo Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza ugonjwa huo pia umepiga hodi Kilimanjaro baada ya mkoa huo kuripoti mgonjwa wa kwanza.

“Hivyo, hadi kufikia leo jumla ya watu 88 wamepata maambukizi ya COVID-19 nchini kutoka 53 tuliowatolea taarifa awali. Ongezeko hili la wagonjwa linajumuisha wagonjwa wapya sita waliotolewa taarifa na Waziri wa Afya Zanzibar mapema leo 15 Aprili 2020,” amesema Mwalimu katika taarifa iliyotolewa na wizara leo jioni Aprili 15.

Amesema hadi sasa wagonjwa waliopona ni 11 na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimefikia vinne.


Soma zaidi: 


Mwalimu amesema Serikali inaendelea kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama wanavyopatiwa taarifa na elimu mara kwa mara.

“Katika kipindi hiki ni muhimu kwa wananchi kuepuka misongamano na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima,” amesema waziri huyo.