Corona yawaibua wabunifu wa mashine za kunawia mikono Tanzania
Wamebuni mashine ya kunawia mikono inafunguliwa kwa kutumia miguu na hautumii nguvu nyingi.
Ubunifu huo umedhamiria kuepusha maambukizi ya Corona kutokana na kufunga na kufungua koki ya bomba.
- Wamebuni mashine ya kunawia mikono inafunguliwa kwa kutumia miguu na hautumii nguvu nyingi.
- Ubunifu huo umedhamiria kuepusha maambukizi ya Corona kutokana na kufunga na kufungua koki ya bomba.
- Teknolojia hiyo inakuja kwa ujazo tofauti kukidha mahitaji ya kila eneo.
Dar es Salaam. “Huwa napata ukakasi pale nikienda buchani kununua nyama nakuta bomba nifungue ninawe na kisha nifunge. Huwa najiuliza kama niko salama kwa sababu linashikwa na watu wengi.”
Ni swali analojiuliza mkazi wa Boko jijini Dar es Salaam, Mediatrice Raphael.
Raphael na watu wengine bado wanakumbwa na taharuki ya kupata maambukizi ya virusi vya Corona wakati wakitumia vifaa kama bomba za kunawia mikono zilizopo katika maeneo ya umma.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuuwa virusi vya COVID-19 vinaweza kukaa sehemu moja (Surface) kwa saa au siku kadhaa kutegemeana na hali ya hewa (joto au unyevu nyevu) na malighafi za eneo husika.
Hivyo hata koki ya bomba za maji zinazotumiwa katika maeneo ya umma zinaweza kusababisha maambukizi ikiwa zimeshikwa na mgonjwa bila kusafishwa.
Suluhisho limepatikana
Kutokana na Changamoto hiyo, Mhandisi wa mitambo na mbunifu wa vifaa chuma Godson Swai ameiona hiyo kama fursa na hivyo kubuni mashine ya kunawia mikono isiyotumia umeme wala chanzo chochote cha Nishati.
Swai ambaye alikuwa akizungumza na Nukta (www.nukta.co.tz) amesema ubunifu huo hakupenda utegemee nishati kwani mtu anashauliwa kunawa mara kwa mara hata kama umeme au nishati hakuna.
Mashine ya kunawia mikono ambayo inatumia miguu kupumpu maji na sabuni wakati wa kunawa. Picha| Mhandisi Swai.
Mashine hiyo yenye tanki la maji badala ya kufunguliwa kwa mikono, inafunguliwa kwa mguu ambapo mtu atakanyaga sehemu maalumu na kama ajabu, atapata sabuni na kisha maji bila hata ya kutumia mikono.
“Kuna sehemu ukikanyaga lile bomba unaliona linatoa maji. Sehemu ya kwanza unakanyaga, sabuni inakunyunyuzia kwenye mikono. Unaenda kwenye koki ya maji unakanyaga inatoa maji,” amesema Mhandisi Swai.
Mashine hiyo imetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu tofauti kulingana na eneo walilopo.
Zinazohusiana:
Swai amesema mashine hiyo inakuja kwa ukubwa wa tanki la lita 250 linalouzwa kwa Sh750,000 huku lita 100 ikiuzwa kwa Sh450,000 na lita 20 likiuzwa kwa Sh175,000.
“Mashine ya lita 250 unaweza kuweka kwenye mashule, hotelini, hospatali na sehemu yenye mikusanyiko mingi kama stendi. Mashine ya lita 20 inaweza kutumika hata majumbani,” amesema Swai.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mashine hizo zikitumika zinaweza kuwaondoa hofu wateja na jamaa zako kwani hawatawaza kuhusu maambukizi kwani inatumia miguu kufanya kazi.
Swai amesema watu walioona teknolojia hiyo wameifurahia na mapokeo ya mashine hiyo hayakatishi tamaa.
Baadhi ya mashine zenye ndoo za kunawia mikono zilizotengenezwa na Mhandisi Swai. Picha| Mhandisi Swai.