CAG aibua utata mkataba wa matunzo ya magari bohari ya dawa
Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini Tanzania imetakiwa kuzingatia bajeti na kanuni za manunuzi baada ya kubaini ilifanya malipo ya takriban Sh1 bilioni kwa mzabuni bila kupata huduma inayohitajika.
- Ni baada ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD)kufanya malipo ya takriban Sh1 bilioni kwa mzabuni bila kupata huduma inayohitajika.
- Mzabuni huyo ni kampuni ya Toyota Tanzania ambaye alitakiwa kutoa huduma ya matunzo ya magari aina ya Land Cruiser.
Dar es Salaam. Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere ameitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini Tanzania kuzingatia bajeti na kanuni za manunuzi baada ya kubaini ilifanya malipo ya takriban Sh1 bilioni kwa mzabuni bila kupata huduma inayohitajika.
CAG Kichere katika ripoti yake kuhusu mashirika ya umma kwa mwaka 2018/2019 amesema Agosti 21, 2018, MSD iliingia mkataba na kampuni ya Toyota Tanzania Ltd kwa ajili ya kutoa huduma ya matunzo ya magari aina ya Land Cruiser ya bohari kwa gharama za Sh996.56 milioni.
Matunzo hayo yangefanyika kwa mkataba wa muda kutegemea kipi kitatangulia kati ya hivi viwili yaani, kipindi cha miaka mitatu au hadi gari litakapotembea kilomita 75,000 kuanzia pale ilipoanza kupatiwa huduma.
Lakini baada ya uhakiki wa maendeleo ya utekelezaji wa mkataba, CAG amebaini kuwa MSD imefanya malipo ya kiasi cha Sh996.57 kwa Toyota Tanzania Ltd kabla ya kupokea huduma kutoka kwa mzabuni kwa kufuata kipengele Na. 4 cha mkataba.
Kanuni za manunuzi ya umma zinaitaka taasisi inayofanya manunuzi kufanya malipo ya manunuzi ya bidhaa au huduma pale inapokuwa imepokelewa na kukubaliwa.
Pia, amebaini kuwa gharama za mkataba zilikuwa zaidi ya bajeti kwa kiasi cha Sh446.5 milioni na hakukuwa na bajeti ya ziada kwa ajili ya manunuzi hayo.
Soma zaidi:
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
- UDSM, SUA, Mzumbe vyadakwa na nyavu za CAG
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Amesema hiyo ni kinyume na Kanuni Na. 224 ya Kanuni za Fedha za Bohari Kuu ya Dawa za Mwaka 2011, inayosema mkurugenzi atahakikisha manunuzi yaliyopendekezwa yako kwenye bajeti na ni sehemu ya mpango wa manunuzi wa taasisi kabla ya kuthibitisha manunuzi yeyote yale.
“Aidha, nilibaini kwamba hakukuwa na ushahidi kwamba mafunzo yalitolewa kwa madereva wa Bohari na mzabuni kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 kama ilivyoainishwa katika mkataba,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa hiyo ni kinyume na mkataba unaosema Toyota Tanzania Ltd itawapatia bure mafunzo madereva wa bohari kwa kuwaongezea ujuzi katika udereva na hivyo kuweza kuepuka kutumia magari vibaya.
Mafunzo hayo yangetolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, na Mbeya. Hata hivyo,
CAG amependekeza Bohari Kuu ya Dawa ihakikishe mafunzo yanatolewa kwa madereva kama ilivyoanishwa kwenye mkataba na ifuatilie kwa karibu huduma itolewayo na mzabuni kuhakikisha inakuwa bora kwa muda wote wa mkataba.