October 6, 2024

Zanzibar yaripoti wagonjwa wengine wawili wa Corona

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya wawili wa virusi vya Corona (#COVID19) na kufanya visiwa hivyo kuwa na wagonjwa tisa mpaka sasa.

  • Wagonjwa wote wawili ni vijana, Watanzania na hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni.
  • Mpaka sasa Zanzibar imefikisha idadi ya wagonjwa tisa kati ya 27 waliopo Tanzania. 

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya wawili wa virusi vya Corona (#COVID19) na kufanya visiwa hivyo kuwa na wagonjwa tisa mpaka sasa.

Mohamed katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 10, 2020) amesema kati ya sampuli walizopeleka jana maabara mbili zimekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

“Hivyo inafanya idadi ya wagonjwa wetu jumla kuwa tisa, kuna ongezeko la wagonjwa wawili wapya,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Ongezeko la wagonjwa hao wawili wa Zanzibar linafanya Tanzania sasa kuwa wagonjwa 27 wa Corona ambapo mmoja amefariki dunia huku watano wakipona.

Mohamed amesema wagonjwa wote wawili ni Watanzania na hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni.

Mgonjwa wa kwanza ni Mtanzania (33) mkazi wa Mwanakwerekwe aliripotiwa Aprili 7 akisumbuliwa na homa kali, mafua na kifua, baada ya kuchukuliwa kipimo alionekana na maambikizi.

Amesema kwa sasa mgonjwa huyo anapatiwa matibabu katika kituo maalum cha Kidimni visiwani huo. 

Mgonjwa pili ni Mtanzania (24) mkazi wa Mtendeni Zanzibar aliyeripotiwa kuwa ana kikohozi na mafua ambapo baada ya kipimo aligundulika ana maambukizi na anaendelea kupatiwa matibabu.


Zinazohusiana:


Aidha, Mohamed amesema hadi jana (Aprili 9, 2020) saa 8:00 Mchana watu 86 waliokutana na watu walioambukizwa Corona wanafuatiliwa huku wengine 252 waliorudi nchini kutoka nje ya Tanzania wamewekwa karantini Pemba na Unguja. 

“Watu 202 wameruhusiwa kutoka karantini baada ya kukaa siku 14 na kutoonyesha dalili za maradhi hayo,” amesema waziri huyo.

 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya. 

Pia wanakumbushwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hasa katika masoko na vituo vya daladala.