Fanya haya wakati wa kununua bidhaa kuepuka Corona
Baadhi ya mambo yatakayokusaidia ni kununua bidhaa mtandaoni na kukaa umbali wa mita moja na muuzaji.
- Baadhi ya mambo yatakayokusaidia ni kununua bidhaa mtandaoni na kukaa umbali wa mita moja na muuzaji.
- Epuka kwenda katika maduka na masoko yenye msongamano mkubwa wa watu.
- Usisahau kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kugusa mdomo, pua au macho.
Dar es Salaam. Janga la Corona bado linaendelea kuumiza vichwa vya viongozi na wananchi huku kila mmoja akitafuta namna ya kujikinga na ugonjwa huo unaotambulika kama COVID-19.
Baadhi ya maduka na masoko katika nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo yamefungwa huku mengi yaliyofunguliwa yakiendeshwa kwa masharti makubwa kuwaepusha watu na mikusanyiko isiyo ya lazima.
Kwa Tanzania bidhaa na mahitaji ya nyumbani yanaendelea kuuzwa lakini ni vyema kuchukua tahadhari ili kuzuia maambukizi kufikia viwango vya mataifa yaliyoathirika zaidi kama Italia, Hispania na Marekani.
Hizi ni baadhi ya dondoo zinazoweza kukusaidia kufanya manunuzi ya bidhaa au kupata huduma katika kipindi hiki ambacho mlipuko wa virusi vya Corona unaendelea kusambaa kwa kasi duniani:
Usiende sehemu zenye msongamano mkubwa
Ingawa hili linaweza kuwa gumu hasa katika majiji makubwa ambayo kwenye mabasi na masoko utakutana na watu wengi, lakini jitahidi kufanya manunuzi yako sehemu ambazo zina watu wachache.
Hii itakusaidia kuepuka mikusanyiko ya watu wengi na kugusana na watu hata ambao huwajui.
Wataalam wa afya wameshauri na wanazidi kusisitiza kuwa watu wanapaswa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ili kuepuka maambukizi ya Corona.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
Usikaribiane sana na watu
Ukienda dukani au sokoni, epuka kukaribiana sana na watu (Close contact) ikiwemo kukumbatiana au kushikana mikono. Umbali unaopendekezwa ni kukaa mita 1 kati ya mnunuzi na muuzaji.
Hii husaidia kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema umbali huo wa mita moja unazuia mate, makamasi au makohozi kumfikia mtu mwingine.
— Ummy Mwalimu, MP (@umwalimu) April 3, 2020
Fanya manunuzi peke yako
Hii inawahusu zaidi wazazi ambao wamekuwa na mazoea ya kwenda na familia nzima kwenye maduka makubwa kununua mahitaji. Katika kipindi unashauriwa kuwaacha watoto wako nyumbani. Nenda pekee yako ili ukawaletee mahitaji wanayotaka.
Kwanini? Hii itasaidia kupunguza idadi ya watu wanaotembelea maduka makubwa au masoko na hivyo uwezekano kupunguza uwezekano wa kukaribiana na watu wengine.
Tumia usafiri binafsi au wa kukodi
Kutokana na ukweli kuwa usafiri wa umma na vituo vya daladala huwa na watu wengi na kusababisha msongamano na kugusana, kama umebarikiwa kuwa na uwezo, unashauriwa kutumia gari lako wakati unaenda kununua mahitaji yako.
Kama hauna unaweza kutumia magari ya kukodi kama Uber na Bolt ili kuepuka kugusana hasa wakati kuingia kwenye gari, japokuwa tayari Serikali imetoa maelekezo kuwa daladala hazipaswi kujaza watu.
Kama itatokea unatumia usafiri wa umma, ni vema kuwa makini na epuka kugusana au kugombania magari.
Gari lako binafsi au la kukodi litasaidia kukuepusha na msongamano wa watu. Picha|Mtandao.
Nunua mtandaoni
Hii ni njia rahisi kabisa kwa sababu kwa kutumia simu yako ya mkononi iliyounganishwa na progrmu tumishi za maduka ya mtandaoni, unaweza kununua bidhaa na ikakufikia mpaka mlangoni kwako.
Kaa nyumbani na agiza chochote utaletewa. Hii ni njia rahisi na bora ya kujikinga na Corona.
Hata hivyo, dondoo hizo hazitakuwa na maana kama hautazingatia miongozo ya wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kugusa mdomo, pua au macho.
Lakini pia epuka mikusanyiko isiyo ya lazima na tumia tishu wakati wa kukohoa.