October 6, 2024

Mgonjwa wa tatu wa Corona apona Tanzania

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kuwa mgonjwa mwingine aliyekutwa na virusi vya Corona mkoani Kagera amepona na kufanya idadi ya waliopona kufikia watatu mpaka sasa.

  • Ni yule aliyegundulika kuwa na maradhi hayo mkoani Kagera.
  • Mpaka sasa waliopona ni watatu na mmoja amefariki dunia.
  • Wananchi watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kuwa mgonjwa mwingine aliyekutwa na virusi vya Corona mkoani Kagera amepona na kufanya idadi ya waliopona kufikia watatu mpaka sasa. 

 “Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3,” ameandika Ummy katika ukurasa wake wa Twitter na kuwa mgonjwa huyo ameruhusiwa kurudi nyumbani. 

Mgonjwa huyo mwanaume anayejishughulisha na udereva wa magari makubwa aliingia nchini kupitia mpaka wa Kabanga na shughuli zake anafanyia kati ya Burundi, Congo DRC na Tanzania alikutwa na  maambukizi hayo Machi 26, 2020. 

Licha ya Tanzania kuthibitisha visa 20 vya wagonjwa wa Corona, Waziri huyo amesema leo Aprili hakuna kisa kipya cha mgonjwa wa Corona. 

Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo una visa vingi vya wagonjwa wa Corona wanaofikia 12 ikifuatiwa na visiwa vya Zanzibar (5), Arusha (2) na mmoja wa Kagera ambaye tayari amepona. 

Kati ya wagonjwa hao waliothibitishwa kuwa na Corona, mmoja kati yao ambaye alikuwa jijini Dar es Salaam amefariki dunia. 


Zinazohusiana


Ummy amesema mgonjwa mmoja wa Arusha, vipimo vyake vya siku tisa vinaonyesha hana maambukizi tena ya ugonjwa huo (Negative) na atapimwa tena siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona kabla hajaruhusiwa kurudi nyumbani. 

Wagonjwa 15 waliobaki hali zao zinaendelea vizuri ambapo Serikali inaendelea na juhudi za kudhibiti ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani. 

Pia Wizara ya Afya imesema watu 40 wameweka karantini katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Horohoro kufuatia kutolewa kwa waraka wa pili wa Serikali wa kudhibiti maambulizi ya virusi vya #Corona mipakani ambao umeelekeza madereva wote wa malori yanayosafirisha bidhaa nje ya nchi wakae karantini siku 14.

Wananchi wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kutokugusa pua, mdomo au macho, na kutumia tishu wakati wa kukohoa na kupiga chafya.