Watoa huduma za intaneti wanavyopambana na Corona
Hatua hiyo inayolenga kuendeleza ufanisi wa wafanyakazi imeanza kutolewa na kampuni za simu za mkononi na intaneti zikiwemo za Liquid Telecom na Vodacom.
- Wametoa ofa na punguzo la bei la vifurushi vya intaneti ili kuwasaidia watu wanaofanyia kazi nyumbani.
- Pia wanafunzi wanawezeshwa kusoma mtandaoni kupitia mifumo ya kimataifa.
Dar es Salaam. Kampuni zinazotoa huduma ya intaneti nchini Tanzania zimeanza kuongeza ufanisi na kupunguza bei ya vifurushi vya intaneti ili kuwapunguzia gharama wafanyakazi wanaofanyia kazi nyumbani kutokana kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya Corona.
Kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo, baadhi ya taasisi na kampuni zimefunga ofisi na kuwaruhusu wafanyakazi kufanyia kazi nyumbani lakini changamoto inayowakabili upatikanaji wa intaneti ya uhakika kukamilisha majukumu yao mtandaoni.
Hatua hiyo inayolenga kuendeleza ufanisi wa wafanyakazi imeanza kutolewa na kampuni za simu za mkononi na intaneti zikiwemo za Liquid Telecom na Vodacom.
Akizungumza na www.nukta.co.tz Mkurugenzi Mkuu wa Raha Liquid Telecom Hussein Kitambi amesema wametoa ofa ya mwezi mmoja ya punguzo la bei ya vifurushi vya intaneti kwa wateja wao.
Liquid Telecom imesema kupitia ofa hiyo, mtumiaji anaweza kupata intaneti isiyo na kikomo yenye kasi ya megabaiti tano kwa sekunde (5MBps) kwa Sh100,000 itakayodumu kwa masa 48.
“Ofa hii itakuwepo kwa mwezi mmoja tu, hata hivyo, tutaendelea kufuatilia hali hii tukiwa pamoja na kukushauri ipasavyo,” amesema Kitambi.
Kupitia ofa hiyo, wafanyakazi wanaweza kufanya kazi kwa uhuru bila shida ya kupungua kasi ya intaneti.
Pia wazazi wanaweza kuitumia kupakua nyenzo za masomo za watoto wake zikiwemo video za kujifunzia na vitabu vya mtandaoni.
Zaidi, kasi ya intaneti hiyo inaweza kumsaidia kwenye kupakua filamu mbalimbali za kujifunzia watoto wa shuleni na hata mtaala mzima wa kimataifa.
Zinazohusiana
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Mifumo ya kidijitali itakayokusaidia kufanya kazi nyumbani
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Hisham Hendi amesema
Vodacom imesaidia huduma ya intaneti kwa kitengo maalum cha Serikali kinachoshughulikia mlipuko wa COVID-19 katika maeneo mbalimbali na kuwawezesha kuwa na mawasiliano wakati wote.
Lakni pia kampuni hiyo ya simu haijabaki nyuma katika kuwapunguzia makali ya maisha Watanzania katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona.
“Tunaweka juhudi za pamoja, kuwasaidia wanafunzi ambao kwa sasa wamefunga shule ili waweze kupata nyenzo za kujisomea kwa njia ya kidijitali kwa kutumia mitaala inayokubalika kimataifa,” amesema Hendi.
Kupitia mfumo uliopitishwa kimataifa wa Khan Academy wanafunzi ambao wako nyumbani kutokana na janga hili wanaweza kuendelea kujisomea wakiwa mtandaoni.
Mpaka sasa, Tanzania imethibitisha visa 20 vya wagonjwa wa Corona ambapo mgonjwa mmoja amefariki dunia na wawili wamepona.
Na pia kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, Jumla ya watu 823,626 wana maambukizi ya ugonjwa huo huku watu 40,598 wakipoteza maisha hadi jana Aprili1, 2020.