October 8, 2024

Corona kuporomosha uchumi wa dunia

Umoja wa Mataifa (UN) umesema uchumi wa dunia unaweza kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka huu wa 2020 kutokana na janga la virusi vya Corona (COVID-19) ukichagizwa zaidi na kushuka kwa uzalishaji wa dunia na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na baadhi ya nchi i

  • Umoja wa Mataifa (UN) umesema uchumi wa dunia unaweza kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka huu wa 2020.
  • Umesema vikwazo vya watu kukutana vinaathiri sekta za huduma na uzalishaji bidhaa. 
  • Jitihada zaidi zinatakiwa ziongezwe kudhibiti virusi vya Corona. 

Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umesema uchumi wa dunia unaweza kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka huu wa 2020 kutokana na janga la virusi vya Corona (COVID-19) ukichagizwa zaidi na kushuka kwa uzalishaji wa dunia na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na baadhi ya nchi ikiwemo Marekani. 

Ripoti iliyotolewa na Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na masuala ya kijamii (DESA) jana Aprili 1, 20-20, imesisitiza kuwa kuongezeka kwa vikwazo vya watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na vikwazo vingine vya Ulaya na Marekani vinaathiri vibaya sekta za huduma hususan viwanda ambavyo vinahusiha watu kukutana kama vile maduka, masuala ya starehe, huduma za mahoteli na usafiri.

“Kwa pamoja sekta hizi zina zaidi ya robo ya ajira zote za kiuchumi. Wakati biashara zikipoteza pato, ukosefu wa ajira unatarajiwa kuongezeka na hivyo kuathiri usambazaji wa bidhaa na mahitaji hali ambayo inaathiri  uchumi,” imeeleza ripoti hiyo. 

Nchi zinazoendelea hasa za Afrika ikiwemo Tanzania ambazo zinategemea sekta ya utalii na usafirishaji nje wa bidhaa huenda zikaathirika zaidi na kuporomoka kwa uchumi wa dunia. 

“Kuporomoka kwa kipato kitokanacho na bidhaa na kubadilika kwa uingiaji wa mitaji ni ishara ya ongezeko la madeni kwa wengi ambao uchumi wao unategemea bidhaa,” imeeleza ripoti hiyo.


Zinazohusiana


Ripoti hiyo imeweka bayana kuwa Serikali huenda zikalazimika kupunguza matumizi ya umma katika wakati ambapo wanahitaji kuongeza matumizi ili kudhibiti kusambaa kwa mlipuko wa virusi na kusaidia matumizi na uwekezaji.

Mkakati mzuri wa kichocheo cha fedha, kuweka kipaumbele katika matumizi ya kiafya ili kudhibiti maambukizi ya virusi na kutoa msaada wa kipato kwa ajili ya kaya zilizoathirika sana na COVID-19 kunaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa mdororo wa uchumi  wa kiwango kikubwa.

“Hatua za haraka na madhubuti za kisiasa zinahitajika sio tu kwa ajili ya kudhibiti janga hili na kuokoa maisha, lakini pia kwa kulinda wale wasiojiweza katika jamii zetu kutokana na mdororo wa uchumi na kusaidia ukuaji wa uchumi na utulivu wa kifedha,” amesema Mkuu wa DESA, Liu Zhenmin.