November 24, 2024

Haya ndiyo masoko ya kuku wa kisasa Tanzania

Jessica ambaye pia ni mwanamuziki wa nyimbo za injili anasema kila anapozalisha kuku wake hana mashaka kwa sababu anaelewa kuwa “masoko ya hawa kuku huwezi kuyamaliza.”

  • Masoko hayo ni pamoja na migahawa, maduka makubwa na madalali wa wafugaji
  • Kuyapatia masoko haya unahitaji uaminifu na kujipanga.
  • Lakini uwe tayari kukabiliana na chamgamoto za usafirishaji na mabadiliko ya hali ya hewa.

Dar es Salaam. Ufugaji wa kuku wa kisasa imekuwa ni biashara inayokimbiliwa na watu wengi lakini siyo wote wanaofanikiwa kwa sababu ya kutokufuata masharti ya wataalam wa mifugo. 

Lakini pia ni ufugaji unaohitaji uwekezaji unaoleweka ili kukabiliana na changamoto mbalimbali hasa magonjwa na vyakula vya kuku na kupata faida inayokusudiwa. 

Waliowekeza nguvu zao na kuzingatia utaalam wa ufugaji, hakika ufugaji wa kuku umewatoa kutokana na kuwepo kwa masoko mengi ya ndege hao ambao hutumika zaidi kama kitoweo cha nyumbani na kwenye mikusanyiko ya watu. 

Mkurugenzi wa kampuni ya JSisters, Jessica Mshama ambaye ni mfugaji wa kuku wa kisasa ni miongoni mwa watu ambao tabasamu hawaliwaishi usoni kila wanapowaangalia kuku katika mabanda yao.

Jessica ambaye pia ni mwanamuziki wa nyimbo za injili anasema kila anapozalisha kuku wake hana mashaka kwa sababu anaelewa kuwa “masoko ya hawa kuku huwezi kuyamaliza.” 

Jessica ambaye alianza na mtaji wa Sh750,000 amesema alianza kufuga kuku 500 miaka mitatu iliyopita na amekuwa akiongeza idadi siku hadi siku kwani hadi sasa idadi ya kuku anaofuga imeongezeka mara 10.

Kama wewe ni mfugaji na unatafuta masoko ya kuku basi haya ndiyo maeneo yatakayokutoa kimaisha:

1. Masoko makubwa

Jessica amesema kuna masoko mengi na kama ukienda sehemu ya kuku, huwezi kukuta “watu wamekauka” ni lazima utakuta huyu anachinjiwa na yule anachagua.

Kwa mujibu wa Binti Mshama, unatakiwa kufanya mazungumzo na wauza kuku pale kuku wako wanapokaribia ili wakiwa tayari, wasiangazie kwa wafugaji wengine.

“Ukiongea nao mimi nina kuku kiasi hiki, wao wenyewe watakua wanakuulizia kuku vipi, tayari?” ameelezea mfugaji huyo ambaye masoko ya Tegeta Nyuki na Bunju jijini Dar es Salaam yanafurahia huduma zake.

Masoko ya kuku wa kisasa huwezi kuyamaliza. unaweza angazia masoko makubwa na hata watu binafsi. Picha| Wadau wa habari.

2. Migahawa

“Nikiitaja sasa si kutafuta wapinzani huko, lakini kila hoteli inayopika chakula ni sehemu ya soko la mfugaji yeyote. Cha msingi usiwe mbabaishaji.

“Siyo unaenda alafu una kuku mia. Wenzio kila siku wanapika sasa hao mia utawapeleka kwa muda gani? Fuga kuku wengi na masoko utakuwa unachagua tu,” amesisitiza Jessica.

3. Wauza chipsi mitaani

Huenda hili lipo wazi lakini unafahamu mahitaji ya hawa jamaa? Kama una alama ya kiulizo, jibu lipo hivi;

Wauza chips wengi wanapenda kuku wa uhakika na zaidi kama ukiwa mfugaji endelevu ni kati ya wateja wazuri watakaoendelea kukutafuta kwa ajili ya huduma yako.

Jessica amesema “Unaweza ukaanza hata na mtaa mmoja ukawa unawapelekea. Kama kuku wako ni wakubwa, watakutafuta kila siku.” 


Zinazohusiana


5. Kuuza kwenye maduka makubwa

Hili ni soko ambalo daktari wa mifugo kutoka kampuni ya Bytrade Tanzania Limited, Dk Christowelu Zephania ameitaja kama soko lenye tija.

“Ukiwafuga kuku wako vizuri ukipeleka kwenye super market (maduka makubwa) kama unavibali na vigezo vyote hawawezi kukukatalia,” amesema DK Zephania.

Ufahamu nini kingine? Pengine ni changamoto ambazo unaweza kuzitarajia kwenye masoko yako. Kwa mujibu wa Jessica, changamoto zilizopo ni pamoja na gharama za usafirishaji na hali ya hewa.

Hata hivyo, amesema kama una uaminifu na mipango mikakati iliyosimama, huwezi kuziona kama changamoto kubwa.

“Mfano kama una gari lako au dereva unayemuamini, unaweza rahisisha usafiri wako na kama banda lako liko vizuri, shida ya hali ya hewa haiwezi kukusumbua kwani litakuwa limejengwa kukabiliana na mvua na mengineyo,” amesema Jessica ambaye kuku wake anawafuga Bagamoyo katika mkoa wa Pwani.

Hata hivyo, Dk Zephania amesema kuwa biashara hii inahitaji uaminifu wa hali ya juu ili kufanikiwa.

“Kama hauna kuku, usimwambie mtu unazo. Ni bora uwe muwazi umwambie ninakutafutia kwa wengine ili hata ukikosa inakuwa siyo shida sana,” amesema daktari hiyo.