October 6, 2024

Dhahabu yachangia kupaa mauzo ya bidhaa nje ya nchi Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika mwaka ulioishia Januari 2020 imeongezeka kwa asilimia 16.6 yakichagizwa zaidi na kupaa kwa bei ya bidhaa katika soko la dunia na kuongezeka kwa kiwango kilichouzwa nje.

  • Mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi yalipaa hadi Dola za Marekani 9.91 bilioni kutoka dola 8.26 bilioni ndani ya mwaka mmoja.
  • Kuongezeka kwa thamani ya bidhaa zisizo za mazao na huduma ikiwemo dhahabu na bidhaa za viwandani kulichangia kupaa kwa mapato. 

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika mwaka ulioishia Januari 2020 imeongezeka kwa asilimia 16.6 yakichagizwa zaidi na kupaa kwa bei ya bidhaa katika soko la dunia na kuongezeka kwa kiwango kilichouzwa nje.

Mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi hujumuisha bidhaa za mazao na zile zisizo za mazao ikiwemo madini ya dhahabu na almasi. 

Ripoti ya tathmini ya uchumi ya mwezi Januari 2020 iliyotolewa hivi karibuni na benki hiyo imesema kwa ujumla mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi yalipaa hadi Dola za Marekani 9.91 bilioni (Sh22.9 trilioni) kwa kipindi hicho ikilinganishwa na dola 8.26 bilioni (Sh19.2 trilioni) iliyorekodiwa Januari 2019  kutokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa zisizo za mazao na huduma.

“Thamani ya bidhaa zisizo za mazao iliongezeka hadi Dola za Marekani 4.29 bilioni (Sh9.9 trilioni) kwa mwaka ulioishia Januari ikilinganishwa na dola 3.27 bilioni (Sh7.5 trilioni) katika kipindi kama hicho mwaka 2019,” imesema BoT.

Mauzo ya bidhaa zisizo za mazao yaliongezeka isipokuwa almasi, kahawa iliyosindikwa na nyuzi za pamba. 

Dhahabu ni miongoni mwa bidhaa zilizochochea pia ukuaji wa jumla wa mapato yatokanayo na mauzo ya nje ya nchi kwa mwaka ulioshia Januari 2020.


Zinazohusiana:


BoT imesema katika kipindi hicho, mauzo ya dhahabu ambayo yalikuwa zaidi ya nusu au asilimia 53 ya bidhaa zisizo za mazao (non-traditional goods) yaliongezeka kwa asilimia 45.6 hadi kufikia dola 2.27 bilioni (Sh5.3 trilioni).

“Ongezeko la kiwango cha dhahabu iliyouzwa nje kwa kiasi fulani limechochewa na hatua za Serikali katika kusimamia shughuli za madini nchini ikiwemo uanzishwaji wa vituo vya kuuzia madini,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

BoT imesema kuwa uuzaji wa bidhaa za viwandani ikiwemo chuma, nondo na mbolea nje ya nchi nao umepaa baada ya thamani ya mauzo kuongezeka kwa asilimia 19.3 hadi Dola za Marekani 974.9 milioni (Sh2.3 trilioni) Januari 2019 ikilinganishwa na ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Hata wakati mapato ya jumla ya mauzo ya nje ya nchi yakiongezeka, mapato yatokanayo na bidhaa za mazao yameongezeka pia hadi dola za Marekani 935.4 milioni (Sh2.2 trilioni) katika mwaka ulioishia Januari 2020 kutoka dola 591.7milioni (Sh1.4 trilioni) katika kipindi kama hicho mwaka 2019.

“Kuongezeka kwa mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi ya kulichangiwa zaidi na kupaa kwa kiwango kilichouzwa kutokana na hali ya hewa nzuri wakati wa msimu wa mazao hayo,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.