November 24, 2024

Bei ya mahindi yapaa mara mbili Tanzania

Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Januari 2020 ilikuwa Sh92,795.8 ikiwa imepanda kutoka Sh49,011 iliyorekodiwa Januari 2019.

  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Januari 2020 ilikuwa Sh92,795.8 ikiwa imepanda kutoka Sh49,011 iliyorekodiwa Januari 2019.
  • Sababu ya kupanda kwa bei hiyo ni kuongezeka kwa mahitaji ya chakula kutoka nchi jirani na kwa sehemu mahitaji ya ndani.
  • Akiba ya chakula katika ghala la Taifa nayo yapungua.

Dar es Salaam. Wakulima na wafanyabiashara huenda wakaendelea kunufaika na kilimo cha mahindi, baada ya bei ya zao hilo kupanda kwa takriban mara mbili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku ikiiacha maumivu kwa wanunuzi wa chakula mashuhuri nchini.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Februari 2020 (Maonthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Januari 2020 ilikuwa Sh92,795.8 ikiwa imepanda kutoka Sh49,011 iliyorekodiwa Januari 2019 sawa na asilimia 47.2.

Bei hiyo ya January ni sawa ongezeko la takriban mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja. 

“Bei ya mahindi, mchele na maharage imeendelea kupanda mfululizo kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya chakula kutoka nchi jirani na kwa sehemu mahitaji ya ndani na kusababisha kushuka kwa uzalishaji hasa katika kanda ya ziwa na kaskazini katika kipindi cha mwaka 2018/19,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kupanda kwa bei ya mahindi kutawafaidisha zaidi wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo ili kujipatia kipato cha kuendesha familia. 

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.


Zinahusiana: 


Mazao mengine ambayo bei yake imepanda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni mchele kwa asilimia 15.5, maharage (asimilia 26.1) na mtama kwa asilimia 30.5. 

Wakati bei ya mazao hayo ikipanda, bei ya viazi mviringo imeshuka hadi Sh72,527.9 mwezi Januari 2020 kutoka Sh80,484.7 iliyorekidiwa Januari 2019. Na ile ya uwele imeshuka hadi Sh127,849.8 kutoka Sh136,845.5.

Hata hivyo, bei za mazao makuu ya chakula zimekuwa za kupanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji. 

Mathalan, katika mwezi Januari 2020 bei za mazao hayo yote isipokuwa uwele zilipanda ikilinganishwa na mwezi uliotangulia wa Desemba 2019.


Akiba ya chakula yashuka

Wakati bei za mazao makuu ya chakula zikipanda na kushuka, akiba ya chakula katika ghala la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) nayo imepungua katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa Januari 2020 ghala hilo lilikuwa na tani 43,596.7 ikilinganishwa na tani 93,037.2 zilizokuwepo Januari 2019.

Mwenendo wa uhifadhi wa chakula katika ghala hilo ambalo huifadhi chakula kwa ajili ya dharura kama njaa umekuwa wa kupanda na kushuka katika miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya BoT imeeleza kuwa kupungua kwa akiba ya chakula mwezi Januari 2020 kulisababishwa na NFRA kuuza tani 8,901.4 za mahindi kwa wafanyabiashara binafsi, Mpango wa Chakula wa Dunia (WFP) na Idara ya Magereza.

“Hii ilisababisha akiba ya chakula kilichokuwepo katika ghala la NFRA kufikia tani 43,597 mwisho mwa Januari 2020 kutoka tani 52,498 za mwezi uliotangulia (Desemba 2019),” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.